Friday 17 June 2011

KILIMO NDIO MUARUBAINI WA MKUKO WA BEI -- DK. SHEIN.

Kilimo ndio muarubaini wa mfumko wa bei – Dk.Shein

Na Rajab Mkasaba, Ikulu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Dk. Ali Mohamed Shein amehimiza haja ya kuendeleza mashirikiano kwa viongozi wa CCM kwa lengo la kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho.
Dk. Shein aliyasema hayo ukumbi wa Jumba la Mawe Dunga, wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja alipokuwa akizungumza na viongozi wa CCM Wilaya ya Kati, ikiwa ni mfululizo wa ziara zake za kuzungumza na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi.
Dk. Shein alisema viongozi wa CCM wana kila sababu ya kuimarisha mashirikiano yao kwani hiyo ni nguzo pekee ya kukiimarisha na kukiendeleza chama hicho.
Sambamba na hilo, Dk. Shein alisisitiza haja ya kuendedeza amani na utulivu uliopo nchini kwani umejenga sifa kubwa ndani na nje ya Zanzibar.
Dk. Shein alisema amani na utulivu imo katika Sera ya CCM ambayo imewezwa kutekelezwa vizuri na hivi sasa faida yake inaonekana nchini ambapo nchi nyingi duniani zimekuwa zikiisifu Zanzibar kwa hatua yake hiyo iliyofikia.
Aidha, Dk. Shein aliwasisitiza viongozi hao kusimama Ilani ya CCM kwa vitendo na kuwaeleza kuwa serikali imekuwa ikitekeleza Ilani ya CCM kwa kiasi kikubwa katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar.
Dk. Shein pia, aliwataka viongozi hao kufanya kazi kwa mashirikiano kati yao na wanachama wa ngazi za chini na kuwataka kwenda Matawini ili kuweza kuwatumikia wananchi na wanachama wa CCM kwa kuwatatulia kero zao zikiwemo wizi wa mazao, mimba za utotoni na nyenginezo.
Pamoja na hayo Dk. Shein aliwataka viongozi hao kuwashajiisha wanachama wa CCM kulipa ada zao za uanachama wa CCM sambamba na kujenga ari ya kujitolea kwani hali hiyo imepungua kwa kiasi kikubwa.
Dk. Shein alieleza kuwa katika ziara yake aliyoifanya hivi karibuni ya kutembelea Mikoa mitano ya Unguja na Pemba na kuona maendeleo ya mikoa hiyo pamoja na chamngamoto zilizopo ameshuhududia mafanikio makubwa yaliopatikana katika sekta za maendeleo ikiwemo sekta elimu, miundombinu ya barabara, kilimo, afya, na nyengine.
alieleza kuwa kwa upande wa sekta ya kilimo alipata nafasi ya kuzungumza na wakulima na kuwaleleza kuwa changamoto zilizopo katika sekta ya kilimo zitapatiwa ufumbuzi kwa kuazia bajeti ya mwaka huu iliyosomwa leo.
Alieleza kuwa Benki ya Maendeleo ya Kiarabu, imeikopesha Zanzibar fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Jendele hadi Unguja Ukuu n a kusisitiza kwa tatizo la maji tayari milioni 25, zimetengwa kwa ajili ya maeneo mbali mbali zikiwemo za Kaskazini, Wilaya ya Kati na nyenginezo kuahidi ndani ya miaka mitano tatizo hilo litakuwa historia.
Pia alizungumzia juu ya suala zima la migogoro ya ardhi na kuendelea kueleza msimamo wake kuwa tatizo hilo liendelee kutafutiwa ufumbuzi na viongozi wakiwemo wa Mkoa, Ardhi, Masheha na Madiwani na baada ya hapo ndio wapeleke taarifa ngazi za juu.
Viongozi wa CCM pia, aliwataka kusimamia na kufanya kazi na viongozi wa mkoa kwa lengo la kutatua matatizo ya mimba za utotoni na kusisitiza haja ya kupiga vita matatizo ya ubakaji.
Kwa upande wa mfumko wa bei, Dk. Shein alisema kuwa serikali iliyopo madarakani haikupandisha bei ya vyakula na hali hiyo haikuanza katika kipindi hichi cha awamu ya saba na kueleza kuwa Serikali inaandaa mipango ya kupunguza ukali wa maisha kwa wananchi.
Dk. Shein alieleza kuwa mfumko wa bei ni tatizo la dunia nzima na kuwataka viongozi hao wasidanganywe na kauli zisizo na msingi juu ya mfumko wa bei ambalo ni tatizo la dunia nzima ambalo pia huchangiwa na kuongezeka kwa bei ya mafuta
“Mimi natamani vitu vyote kupunguza bei lakini haiwezekani.... Mapinduzi ya kilimo ndio njia moja wapo kubwa katika kupambana na tatizo la chakula ambapo maandalizi makubwa yameandaliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar juu ya hili”,alisema Dk. Shein.
Akieleza juu ya ughali wa bei ya sukari amesema kuongezeka kwa bei yake kumetokana na nchi wanaolima sukari kwa wingi hivi sasa wamekuwa wakijishughulisha na uzalishaji wa spiriti zaidi ya sukari kutokana na kutumia bidhaa hizo kuwa mbadala wa mafuta ya kuendeshea gari hasa nchini Brazil.
Aidha, Dk. Shein alisema uhaba huo umejitokeza hata hapa nchini kutokana na uzalishaji wa sukari kupungua kutokana na uhaba wa viwanda vya kuzalisha bidhaa hiyo ama viwanda vyengine kutozalisha kabisa sukari kama kilivyo kiwanda cha Mahonda hivi sasa.
Dk. Shein alieleza lengo kubwa katika kipindi kifupi kijacho ni kuzalisha kwa kiasi kikubwa mpunga na kufikia kuzalisha tani 40 elfu hapa nchini na lengo ni kulima mpunga hapa hapa Zanzibar.
Aliwasisitiza vijana kukipenda kilimo na kutoa mfano katika shamba la mbegu la Bambi sambamba na kuimarisha sekta ya kilimo ili kufikia lengo la kuzalisha chakula kwa wingi na kuweka akiba.
Aliwaeleza vijana kuwa watakipenda kilimo kwani hatua kubwa zitachukuliwa katika kuhakikisha kilimo kinapata manufaa na kueleza kuwa vijana ipo siku watafurahi kutokana na hatua itakayofikiwa.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alitoa pongezi kwa Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa kwa ziara zake kuwatembelea wanaCCM na kueleza kuwa ziara hizo zinawajengea ari katika kukiimarisha chama chao.
Wakitoa neno la shukurani viongozi hao walieleza kuwa elimu waliyoipata katika hotuba ya Rais Dk. Shein wataitoa kwa wanancnhi wanachama wa CCM.

No comments:

Post a Comment