Friday 10 June 2011

TUNZO ZA WANAMUZIKI BORA KUWANIWA LEO.

Tuzo za wanamuziki bora kuwaniwa leo

Na Mwashungi Tahir, Maelezo
UKUMBI wa Salama ulioko katika hoteli ya Bwawani, leo usiku unatarajiwa kurindima pale wasanii mbalimbali wa muziki watakapokuwa wakiwania tuzo tafauti.
Tamasha hilo ‘Vodacom Zanzibar Music Award’, litapata baraka za kushuhudiwa na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi atakaekuwa mgeni rasmi.
Waandalizi wa hafla hiyo ya kutambua mchango wa wanamuziki bora kwa mwaka 2011 kampuni ya ‘Zanzibar Media Entertainment’, wametaja maeneo mbalimbali yatakayoshindaniwa katika tamasha hilo la sita.
Meneja wa kampuni hiyo inayomiliki kituo cha redio cha Zenj FM na gazeti la Nipe Habari Seif Mohammed Seif, amefahamisha kuwa jumla ya vikundi 18 vya muziki hapa Zanzibar vitashiriki mbali na wasanii mmoja mmoja katika nyanja tafauti.
Nyanja hizo ni pamoja na taarab asilia na ya kisasa, ngoma asilia, muziki wa kizazi kipya pamoja na wa dansi, ambapo pia kutakuwa na tunzo za msanii bora wa kike na wa kiume katika maeneo yote hayo, sambamba na watunzi wa kazi mbalimbali za sanaa ya muziki.
Seif pia alisema, katika kutoa tuzo, waandaaji wa tamasha hilo watawakumbuka wasanii mbalimbali wakongwe pamoja na waliotanglia mbele ya haki ambao wametoa mchango mkubwa katika tasnia ya muziki visiwani humu.
“Maandalizi yote ya tamasha la tunzo za wanamuziki bora yamekamilika, na tunatarajia mwaka huu litakuwa la aina yake, na majaji watafanya kazi kwa kuzingatia namna wasanii walivyopata kura zilizopigwa na mashabiki”, alihitimisha Meneja huyo.

No comments:

Post a Comment