Wednesday 8 June 2011

MKULO AWASILISHA BAJETI YA KUKATA UKULI WA MAISHA.

Mkulo awasilisha bajeti ya kukata ukali wa maisha

• Ni zaidi ya trilioni 13/-
• Miundombinu, Afya, Elimu zaongezewa fedha
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WAZIRI wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mustapha Mkulo amesema bajeti mpya itatoa vipaumbele katika kuhakikisha inatanzua vikwazo vinavyoendelea kuwakabili wananchi katika kupunguza umasikini.
Alisema kutanzuliwa kwa vikwazo hivyo kutawezesha wananchi kuweza kumudu gharama za maisha na kukabiliana na hali ya ngumu ya umasikini ambayo imekuwa ikiwakumba Watanzania.
Waziri Mkulo alieleza hayo jana Bungeni mjini Dodoma, alipokuwa akiwasilisha makadirio ya matumizi na mapato ya serikali kwa mwaka mpya wa bajeti 2011/2012.
Alisema vipaumbele vyengine vitakavyozingatiwa katika utekelezaji wa bajeti hiyo ni pamoja na kuweka mikakati zaidi ya kukusanya mapato ya ndani pamoja na kuhakikisha misamaha ya kodi inapunguzwa.
Mkulo alisema bajeti hiyo utekelezaji wake pia utazingatia malengo ya dira ya maendeleo ya mwaka 2025, mipango ya milenia pamoja na mpango wa maendeleo wa miaka mitano ambao juzi ulizinduliwa na Rais Jakaya Kikwete.
Aidha alisema suala la miundombinu nalo litatekelezwa kikamilifu sambamba na ujenzi wa miundombinu ikiwemo barabara, reli pamoja na bandari ili kurahisishwa uchapuzaji kasi ya ukuaji wa uchumi wa taifa.
Sekta nyengine zilizoongezewa fedha za bajeti katika mwaka mpya ni pamoja na kilimo hasa cha umwagiliaji, maji, elimu pamoja na afya, huku akisema hali hiyo itasaidia kuwaondolewa shida za kimaisha wananchi.
Waziri huyo alilieleza Bunge hilo serikali itahakikisha inasimamia kikamilifu suala la uwajibikaji pamoja na pamoja na kuzijengea uwezo wa rasilimali ambazo ni kichocheo cha ukuaji wa uchumi.
Alisema pamoja na hali ya uchumi wa Tanzania kuwa tulivu na kuanza kutengemaa hivi sasa, bajeti ijayo itaendelea kuwa tegemezi, ambapo utegemezi huo umeshuka kutoka asilimia 28 na kushuka hadi asilimia 17.
Alisema hadi kufikia mwaka 2015, lengo na mipango ya serikali ni kuhakikisha kuwa utegemezi wa bajeti kutoka kwa wahisani unapungua na usizidi asilimia 10.
Katika kuhakikisha serikali inashuhgulikia suala la matumizi yasio na faida, imepanga kupunguza manunuzi ya gari za serikali hadi kwa dharura maalum ambayo itatolewa na ofisi ya waziri Mkuu.
Aidha waziri Mkulo alisema katika bajeti ijayo serikali itapunguza matumizi ya mafuta kwa gari za serikali, safari za nje ya nchi, posho, kupunguza semina, warsha zisizo na tija pamoja na kupunguza kupunguza gharama za maonesho na sherehe.
Alilieleza Bunge hilo kuwa katika mwaka unaomalizika wa bajeti, taarifa za mdhibiti na mkaguzi wa hesabu za serikali zimeonesha kuwa kumekuwepo na ongezeko la hati chafu na kupungua kwa hati safi, ambapo alisema tatizo hilo linatokana na kutofuatwa kanuni na sheria za matumizi umma.
Akizungumzia suala la maslahi kwa watumishi wa umma, alisema serikali itaendelea kuwapatia stahili kwa kuhakikisha kuwa wanamudu gharama za maisha sambamba na kupatiwa fedha za likizo pamoja na haki nyengine muhimu.
Kuhusu mashirika ya umma, alisema pamoja na dhana nzuri ya kuanzishwa kwa mashirika hayo yapo baadhi yamekuwa mzigo baada ya kushindwa kujiendesha na kusababisha kuwa tegemezi kwa ruzuku serikalini.
Katika bajeti hiyo waziri mkulo amepunguza kodi kwenye mafuta mazito ya uendeshea mitambo, na kuongeza kodi katika vinywaji ikiwemo bia, mvinyo pamoja na sigara huku kodi hiyo ikitofautiana baina ya bidhaa zinazozalisha ndani na nje.
Katika bajeti hiyo serikali imepanga kutumia kiasi cha shilingi trilioni 13.2 ikiwa ni kwa kazi za kawaida na utekelezaji wa mipango ya maendeleo, makusanyo yakitarajiwa kufika trilioni 6.7.
Katika hotuba hiyo waziri Mkulo alizipongeza nchi wahisani na mashirika kwa kuisaidia bajeti ya Tanzania, huku baadhi ya nchi hizo zikikabiliwa na matatizo katika nchi hizo.

No comments:

Post a Comment