Friday 10 June 2011

BALOZI SEIF AWAPA VIDOGE WABUNGE

Balozi Seif awapa vidoge wabunge

Awataka waepuke kukitia aibu chama, viongozi
Ashangaa wabunge, wawakilishi kutoelewana
Na Mwantanga Ame
MAKAMU wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi, amewaeleza wabunge wa CCM kukwepa janga la kuwatia aibu viongozi wa chama hicho kwa kuzomewa na kushushwa kwenye majukwaa kwa aibu.
Balozi Seif alisema aibu hiyo inaweza kutokea kwa viongozi wa CCM kushushwa kwenye majukwaa na kuzomewa endapo wabunge hao watashindwa kutekeleza ahadi walizoziweka kwa wananchi.
Makamu huyo alieleza hayo kwenye hafla ya chakula cha usiku iliyofanyika nyumbani kwake mtaa wa Farahani mjini Dodoma, iliyowajumuisha wabunge wa CCM, ambayo ilikuwa na lengo la kubadilishana mawazo.
Alisema aibu hiyo inaweza kuepukwa endapo wabunge hao watatambua wajibu wao wanaotakiwa kuufanya kwa wananchi kwa kuhakikisha wanakuwa watumishi bora sambamba na kuzitimiza ahadi zao.
“Ndugu zanguni msipokuwa makini kwa kutoteleza majukumu yenu, mnaweza kumtia aibu Rais wa Zanzibar kwa kuzomewa ama kushushwa majukwaani pale atakapokuwa anawadi kama wagombea”, alisema.
Balozi aliwaeleza wabunge hao kuwa lazima wazingatie na kulifanyiakazi suala hilo kwani matokeo ya aina hiyo yalionekana katika maeneo mengi kwenye uchaguzi mkuu uliopita, jambo ambalo lilimfanya mgombea wa Urais wa CCM Dk. Jakaya Kikwete, kujikuta kwenye wakati mgumu.
Alisema sababu kubwa ya kujitokeza mambo hayo ilitokana na baadhi ya viongozi waliochaguliwa na wananchi kutoonekana katika majimbo huku ahadi walizozitoa kushindwa kuzifanyia kazi.
Kuwepo kwa hali hiyo Balozi Seif, alisema Chama cha Mapinduzi hakitapenda kuona hali hiyo inajirejea tena katika uchaguzi mkuu wa 015, na ni lazima wabunge na wawakilishi wa CCM, kuhakikisha wanatimiza ahadi zao za kuwatumikia wananchi.
Alisema Chama cha CCM kwa kuthamini wanachama wake wawe katika hali nzuri hivi sasa tayari mfuko wa maendeleo ya Jimbo umeanza kuwapatia wabunge ambazo zitasaidia kuhudumia majimbo ambapo wabunge wote wa Zanzibar wataweza kufaidika nao.
Balozi Seif, alisema nia ya serikali ya Muungano kutoa fedha hizo ni kuhakikisha mahitaji ya wananchi yanatimizwa katika miradi mbali mbali ya maendeleo ndani ya majimbo na sio kutumiwa vyenginevyo hasa kuangalia maslahi binafsi ya Mbunge.
Alisema hivi sasa mkakati ambao watalazimika kuufanyiakazi ni kuhakikisha wanamaliza tatizo la ukosefu wa vikalio katika maskuli yaliopo katika majimbo yao kwani hiyo ni moja ya ahadi ambayo ameitangaza rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein ambapo utekelezaji wake utakuwa unawahusu wabunge na wawakilishi.
Alisema inasikitisha kuona tatizo hilo baadhi ya viongozi wa majimbo bado hawajaweka deski hata moja katika skuli walizonazo kwenye majimbo yao jambo ambalo wanapaswa kuona aibu kwani haipendezi kuendelea kuwaacha wanafunzi kukaa chini maskulini.
Alisema ni jambo la kwani zipo taarifa za baadhi ya wabunge na wawakilishi kutoelewana katika majimbo yao jambo ambalo linahitaji kuepukwa kwani linaweza kukisababishia Chama cha CCM kufanya vibaya katika uchaguzi Mkuu ujao.
Alisema tahadhari lazima ichukuliwe kuhakikisha tofauti walizonazo zinaondoka na kukubali kufanyakazi kwa pamoja, kwani CCM ijayo itahakikisha haitawapa nafasi viongozi wababaishaji kwani imo katika kundaa mpango utakaotumika kupata viongozi katika kura ya maoni.
Hata hivyo Balozi Seif aliwatoa wasi wasi wabunge hao juu ya maendeleo ya matayarisho ya mswaada wa katiba mpya ambapo alisema kuwa tayari yapo katika hatua nzuri na ushiriki wa Zanzibar pamoja na maoni yao yameweza kuwasilishwa namna ya mchakato huo unavyotakiwa uende.
Alisema wanacho subiri hivi sasa ni kuona nini serikali itaamua baada ya mapendekezo hayo kufikishwa mbele ya serikali zote mbili na kuwataka wabunge hao kusubiria matokeo hayo.
Nae Naibu waziri wa Fedha katika Serikali ya Muungano, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Chumbuni, Pereira Silima, akitoa shukrani zake alisema watahakikisha kuwa wanatekeleza wajibu wao kwa kuwatumikia vyema wananchi.
Alisema nia yao ya kuomba kuchaguliwa kuwatumikia wananchi ni kutokana na kuwa na nia ya kuwasaidia kuondokana na matatizo waliyonayo na watahakikisha kuwa wanashirikiana na kuona wanautumia vyema mfuko huo kuondoa matatizo yao.

No comments:

Post a Comment