Mapungufu ya sheria ya ndoa yaanikwa
Na Jumbe Ismailly, Singida
MGANGA mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Robert Salimu amesema sheria ya ndoa ya mwaka 1971 inayoruhusu msichana mwenye umri chini ya miaka 14 kuolewa kwa ridhaa ya wazazi na kuanzia miaka 18 kwa riadhaa yake mwenyewe inachangia ongezeko la watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi kwa kuwa ndoa hizo siyo za hiyari.
Mganga huyo alisema hayo kwenye hotuba ya ufunguzi wa semina ya siku moja ya utambulisho wa mradi wa Pamoja Tuwalee mkoa wa Singida iliyofanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya wananchi (FDC), mjini humo.
Alisema ndoa zinazozalishwa na sheria hiyo siyo tu zinamnyima mtoto haki zake za kimsingi kama vile kupata elimu, kuoa au kuolewa, kuzaa au kutokuzaa, kuchagua mume anayempenda, kukua na kulindwa.
“Ziko sheria na sera zinazokwamisha upatikanaji wa haki za vijana zirekebishwe, mfano sheria ya ndoa ya mwaka 1971 inaruhusu msichana chini ya miaka 14 kuolewa kwa ridhaa ya wazazi na kuanzia miaka 18 kwa ridhaa yake mwenyewe ndoa zinazozalishwa na sheria hii zinamnyima mtoto haki”,alisema.
Alifahamisha kuwa changamoto za vijana hao wanaoishi katika mazingira hatarishi zifanywe kuwa ajenda za kitaifa, kwa kuziingiza kwenye mipango ya muda mfupi na muda mrefu kwa kuwa zinagusa mustakabali wa taifa.
Alisema endapo masuala ya watoto hao yatawekwa kwenye mipango hiyo itawezesha kuwasaidia kuwaepusha vijana kuwa wapagazi na vijakazi wa wawekezaji pamoja na wageni katika ulimwengu wa utandawazi.
Dk. Salimu alisema wakati umefika wa mifumo ya elimu kutazamwa upya ili iweze kuwasaidia vijana katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha baada ya kumaliza masomo yao kama njia ya kupunguza ongezeko la watoto au vijana wanaoishi katika mazingira hatarishi na kuzagaa mitaani bila kazi.
Awali akitoa maelezo mafupi juu ya semina hiyo kwa Mganga mkuu kabla ya ufunguzi wa semina hiyo, Mwezeshaji wa kutoka mkoani Mwanza, Jacinta Mutakyawa alibainisha kuwa vijana walioko kwenye mchakato wa ukuaji wao kwa namna moja au nyingine wamekuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Umati kutoka Kanda ya kaskazini, Fredy Turuka alisisitiza kwamba uwepo wa vijana hao unategemea uwajibikaji wa pamoja wa jamii wa kipindi hiki cha sasa.
“Kwa pamoja kwa nafasi yetu, nadhani tumefika hapa tukiwa tunatambua majukumu na tuna wajibu wa kushirikiana ili tuweze kufanikiwa kiasi fulani na tuupokee pia kwa furaha kwa sababu umetufikia kwenye mkoa wetu na ndani ya mikoa 25 ya Tanzania”, alisema.
Monday, 20 June 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment