Thursday 23 June 2011

DAWA MCHANGANYIKO ZA MALARIA BURE.

Dawa mchanganyiko za malaria bure

Na Mwanajuma Abdi
WAZIRI wa Afya, Juma Duni Haji ameeleza sababu zilizochelewesha Zanzibar kuanza kwa mradi wa upatikanaji wa dawa za mchanganyiko 'artemisinin' za kutibu malaria kwa bei nafuu ulioanza mwaka jana na kumalizika mwaka 2012, ni kutokana upatikanaji wa fedha za uagiziaji dawa hizo na kuziingiza nchini.
Hayo aliyasema jana, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika hoteli ya Zanzibar Ocean View Kilimani, ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa mradi huo, ambapo kitaifa utazinduliwa leo katika viwanja vya Tumbaku, Miembeni mjini hapa.
Mradi huo kwa Zanzibar utatumia shilingi milioni 700 hadi utakapokamilika kwa awamu ya kwanza, ambapo tathmini yake itafanyika Novemba mwaka huu kwa nchi zote nane kwa lengo la kuangalia mafanikio ili nchi nyengine ziweze kuingizwa katika mpango huo awamu nyengine.
Alisema mradi wa upatikanaji wa dawa bora na sahihi za kutibu malaria kwa gharama nafuu ulianza mwaka 2010 na kumaliza mwaka 2012, ambapo nchi nane kutoka katika Bara la Afrika na Asia zimebahatika kuwa miongoni mwa nchi hizo lakini Zanzibar ilishindwa kuanza kwa wakati kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo upatikanaji wa fedha za kuagiza dawa hizo na kuziingiza nchini.
Alizitaja nchi hizo, ni Cambodia, Ghana, Kenya, Madagascar, Niger, Nigeria, Tanzania Bara na Uganda, ambapo na Zanzibar imeingia kama nchi katika mradi huo, unaofadhiliwa na wahisani mbali mbali duniani ambao waliamua kuunganisha nguvu zao kwa pamoja na kuanzisha Mfuko wa Fedha wa Dunia (Global Fund) wa kupambana na UKIMWI, TB, na malaria, ambao mfuko huo unasaidia zaidi ya nchi 100.
"Dawa hizi kimsingi bado zina gharama kubwa kuzinunua, lakini kutokana na makubaliano ya nchi husika zitafaidika na punguzo la takribani asilimia 95 zitalipwa kupitia mfuko wa 'Global Fund' na kufanya dawa ziuzwe kwa gharama nafuu kabisa kwa walengwa na asilimia tano zitalipwa na nchi husika", alisema Duni.
Alieleza dawa za mchanganyiko wa 'artemisinin' zilikuwa zinauzwa kwa bei ya juu baina ya shilingi 6,000 hadi 12,000, jambo ambalo lilisababisha wagonjwa wengi kushindwa kumudu gharama hizo, ambapo kwa sasa katika vituo vya afya vya Serikali zitatolewa bure na katika maduka ya dawa na hospitali binafsi zitauzwa kwa dozi ya mtu mzima isiyozidi shilingi 1,000 na mtoto isiyozidi shilingi mia nane.
Waziri Duni alifafanua kuwa, dawa hizo zina chapa ya alama ya jani lenye maandishi yanayosomeka 'ACTm', ambapo jani hilo linatokana na mti wenyewe asili uliotengenezewa, hivyo jamii ina jukumu na kuhakikisha kuzitambua dawa hizo, sambamba na kuuziwa kwa bei iliyopendekezwa na Serikali na si vyenginevyo.
Alitoa onyo kwa wauza dawa kuwa sio ruhusa kuuza dawa hizo kwa mtu asiyekuwa hana cheti cha daktari, ambapo aliwataka madaktari kufuata maadili yao ili kuepusha uibaji wa dawa hizo katika hospitali za Serikali na kuziuza vituo binafsi kwani atayepatikana na kadhia hiyo atafikishwa katika vyombo vya sheria.
Aidha alitanabahisha kwamba, dawa nyengine mchanganyiko ambazo hazina alama hiyo, zinakubalika kutibu malaria ila hazihusiki katika punguzo la bei hiyo, hivyo bei zake zitategemea na soko huria la dawa.
Duni alitahadharisha kwamba baadhi ya malengo yaliyokuwemo katika mradi huo ni pamoja na kuhakikisha kuwa kila duka la dawa, hospitali na vituo vya afya vya sekta binafsi zinatunza na kuuza dawa hizo kwa bei iliyopangwa, kutunza kumbukumbu zote za manunuzi ya dawa na mauzo kwa ajili ya ukaguzi.
Aliongeza kusema kwamba, mazingatio mengine ni kuruhusiwa kwa wafadhili kukagua na kupewa taarifa ya mwenendo wa mradi huo kwa sekta binafsi na serikalini na kuhakikisha kuwa dawa hizi hazivuki mipaka ya Zanzibar na kuuzwa katika nchi ambazo hazishiriki katika mradi huo kwani kufanya hivyo itakuwa kwenda kinyume na mkataba.
Hata hivyo, alisema ripoti za Shirika la Afya Duniani zinakadiria takribani wagonjwa 225 milioni waliugua malaria mwaka 2009 na idadi ya vifo kutokana na malaria ilikuwa 781,000 kwa dunia mzima.
Alisema kwa Zanzibar tafiti zinaonyesha mwezi Mei hadi Julai mwaka jana takwimu zinasema kiwango cha maambukizi ya malaria kimeshuka hadi kufikia asilimia 0.07 tofauti na takwimu za mwaka 2007 zilionesha asilimia 0.8.
Alifahamisha kuwa, kutokana na ripoti hizo bado malaria ni janga la kimataifa linalozikabili nchi nyingi hasa zinazoendelea kusini mwa jangwa la Sahara, ambao unaendelea kuua maelfu ya watu duniania na hasa watoto wadogo wenye umri wa chini ya miaka mitano na kinamama wajawazito.
Wakati huo huo, Mratibu wa Mradi huo, Shija Joseph alitoa wito wakati akiwafunda wenye maduka ya vituo vya watu binafsi kuhakikisha wanauza dawa hizo kutokana na vigezo vilivyowekwa ili kuwafikishia huduma hiyo wananchi walio wengi na sio kama awali wachache ndio waliweza kumudu gharama za dawa hizo.
Alisema mradi huo unalenga kuwasaidia wananchi na kuokoa maisha ya watu kutokana na ugonjwa hatari wa malaria, ambapo aliushukuru Mfuko wa Fedha wa Dunia kwa kusaidia sehemu kubwa ya gharama za dawa hizo.

No comments:

Post a Comment