Monday 13 June 2011

ICPS KITASAIDIA SEREKALI , WATUMISHI

ICPS kitasaidia serikali, watumishi

Na Khamis Mohammed
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haji Omar Kheir, amesema, kuanzishwa kwa Chuo cha ICPS ni mchango mkubwa sio kwa serikali pekee, bali hata kwa utumishi wa umma hapa nchini.
Alieleza hayo wakati akifungua mkutano wa wadau huko ambao ulijadili mitaala ya chuo hicho cha kuwaendeleza wataalamu Zanzibar hoteli ya Bwawani mjini Unguja.
Alisema, kitendo kilichofanywa na Chuo cha ICPS ni sehemu kubwa ya uzalendo, kwani kujitokeza kwa wazawa na kuwekeza katika elimu kama hizo za kitaalamu ni sehemu ya ujenzi wa taifa kwa kuwapata wataalamu wa kada na ngazi tofauti.
Hivyo, alitoa wito wa kuanzishwa kwa vyuo au taasisi mbalimbali za kielimu hasa katika kada za kitaalamu ili kukisaidia Chuo cha Utawala wa Umma katika kuongeza kasi na mabadiliko ya utumishi na Utawala Bora Zanzibar.
“Hii ni chachu katika kuendeleza na kuanzisha ushindani mwema wa kitaalamu katika uwanja wa elimu ya msingi, cheti, diploma na hata digrii”, alieleza waziri huyo.
Hata hivyo, waziri huyo alisema kuanzishwa chuo au taasisi ni muhimu kuweza kukifanya kuwa rasmi na kutambulika ili kuondosha shaka na wasiwasi kwa wazee, wanafunzi wenyewe na hata serikali kwa ujumla.
Alisema, kuwa na chuo ambacho hakitambuliki situ ni kosa la kisheria, bali pia kunavunja nguvu na mori kwa wanafunzi na wanachuo husika.
Aidha waziri huyo, alisema kuwepo kwa taasisi hiyo ni fursa pekee ya kielimu kwa vijana katika kuongeza utaalamu.
Mapema mwenyekiti wa Bodi ya Chuo hicho, Mohammed Khamis, alisema, changamoto kubwa inayowakabili vijana ni kupata ajira, lakini wanakosa kuajiriwa kutokana na kukosa sifa.
Hivyo kujitokeza kwa chuo hicho kutafungua ukurasa mpya kwa vijana kuweza kujipatia utaalamu na kuingia katika soka la ajira.

No comments:

Post a Comment