Tuesday, 14 June 2011

MADAKTARI WAUZA DAMU KUSHUGHULIKIWA -MAALIM SEIF.

Madaktari wauza damu kushughulikiwa Maalim Seif

Na Mwanajuma Abdi
MAKAMU wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad amesema serikali haitowafumbia macho watumishi wa afya wataojihusisha na uuzaji wa damu kwa wagonjwa pindi wanapoihitaji.
Hayo aliyasema jana, katika sherehe za maadhimisho ya siku ya wachangiaji damu duniani, ambapo kwa Zanzibar zilifanyika katika viwanja vya Ngome Kongwe mjini hapa.
Alisema serikali ya Mapinduzi Zanzibar yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa haitowafumbia macho madaktari wataojihusisha na kadhia hiyo, kwani wanaweza kusababisha kuwapotezea maisha wananchi.
Aliongeza kusema kwamba, madaktari wataobainika kuuza damu nguvu za dola zitatumika kuwadhibiti ili kukomesha vitendo hivyo nchini.
Alisema wazanzibari wanatabia ya kuwaonea muhali watimishi wa afya wenye tabia hiyo, hivyo aliwaaagiza viongozi wa wizara ya Afya kulifuatilia kwa karibu suala hilo.
"Madaktari wanaobainika wanauza damu kwa wagonjwa hatua kali zitachukuwa dhidi yao, na kuiagiza wizara ya Afya isimamie jambo hilo kwa makini", alisisitiza Maalim Seif.
Alieleza wanawake wanapojifungua wengi wao wanapoteza maisha kutokana na kutokwa na damu nyingi wakati wanapojifungua hivyo kuwepo kwa kituo cha damu salama kinasaidia katika kuondosha tatizo hilo.
Aliongeza kusema kwamba, mbali ya kinamama kupoteza maisha lakini watoto waliokuwa chini ya umri wa miaka mitano nao hupoteza maisha kutokana na upungufu wa damu mwilini kunakosababishwa na lishe duni au maradhi nyemelezi ikiwemo malaria nalo huchangia.
Alifahamisha kuwa, mbali ya watoto nao vijana wa kiume hupoteza maisha kutokana na ajali zinazotokea, ambazo zinasababisha kupoteza damu nyingi mwilini.
Alisema kuongezewa damu binaadamu ni tiba tosha ya kumrejesha afya yake katika hali ya uzima, hivyo alitoa wito kwa wananchi kujitolea damu kwa hiari ili iweze kuwepo ya kutosha katika Benki ya Damu na kuwasaidia watu wanapohitajika kuwekewa kwa haraka ili kuokoa maisha yao.
Alifafanua kuwa, malengo ya milenia ni kuhakikisha kunapunguzwa kwa idadi ya vifo vya mama na mtoto, ambapo aliwapongeza Wizara ya Afya kwa kuanzisha kitengo cha uchangiaji wa damu salama, ambayo inachunguzwa maradhi yote ikiwemo UKWIMU, homa ya inni na magonjwa mengine hatarishi kwa binaadamu.
Maalim Seif aliwataka wafanyabiashana na makampuni kuunga mkono jitihada za wachangia damu ili ziwe endelevu katika kuimarisha huduma za afya kwa wananchi nchini.
Aliwapongeza idadi kubwa ya wachangiaji damu nchini kutokana na muamko mkubwa waliupata, hivyo aliwahimiza uwe endelevu na wajilinde na maradhi ya maambukizi kama gonjwa hatari la UKIMWI.
Nae Katibu Mkuu wa Afya, Dk. Saleh Mohamed Jiddawi alisema idadi kubwa ya wachangiaji wa damu ni wanafunzi wa skuli za sekondari, vyuo, vikosi vya ulinzi na usalama, ambapo alikanusha uvumi uliokuwepo kwamba wanaotolewa damu hiyo lishe yao ni duni.
Alieleza mtu hawezi kutolewa damu kama hajachunguzwa afya yake na kuulizwa historia ya maradhi kama pumu, kifafa, sukari na presha sambamba na kuangaliwa kiwango chake cha damu ili asiweze kupata matatizo.
Mkurugenzi Mkuu wa Afya, Dk. Malik Abdulla Juma alitilia mkazo kwa wananchi wasikubali kuuziwa damu kwa ajili ya kuongezewa wagonjwa wao, ambapo wakilazimishwa waende kutoa ripoti ili daktari huyo achukuliwe hatua.
Aliongeza kusema kwamba, hali ya uchangiaji damu umeimarika zaidi katika kipindi hiki ukilinganisha na miaka 10 iliyopita kutokana na wananchi kupata muamko mkubwa wa kujitolea kuchangia.
Mapema Meneja Mpango wa Damu Salama Zanzibar, Dk. Mwanakheri Ahmed alifahamisha kuwa, watu wanaohitajika kuchangia damu ni kuanzia umri wa miaka 18 hadi miaka 65 pamoja na uzito kuanzia kilo 50.
Alisisitiza kuwa, watumiaji wakubwa ya damu hiyo ni wodi ya wazazi, watoto na chumba cha upasuaji kwa ajili ya kuokoa maisha ya akinamama na watoto.
Nae Katibu wa Jumuiya ya Wachangiaji damu Zanzibar (JUWADAHIZ), alifahamisha kuwa, hivi sasa jumuiya hiyo inawanachama 800 Unguja na Pemba, ambapo tatizo kubwa linalowakwanza ni ukosefu wa fedha za nauli pindi wanapohitajika kwenda kuchangia damu kwa wagonjwa hususani wa makundi adimu hivyo wamewaomba wafadhili na watu mbali mbali wawachangie.
Katika sherehe hizo, Maalim Seif aliwakabidhi zawadi wachangiaji mbali mbali ikiwemo Farid Mohamed aliyechangia kwa mara 22, Hussein Ali mara 22, Hadaa Khatib mara sita, ambae ni mama mlemavu, skuli za sekondari, vikosi vya ulinzi na usalama, vilabu vya michezo ya viungo na jumuiya hiyo.

No comments:

Post a Comment