Wednesday, 15 June 2011

WAZIRI DUNI AIELEZA UN MAFANIKIO AFYA TANZANIA

Waziri Duni aieleza UN mafanikio afya Tanzania

Na Mwandishi Maalum, New York
RAIS wa Baraza Kuu la 65 la Umoja wa Mataifa Joseph Deiss amesema Tanzania ni nchi ya kupigiwa mfano katika utoaji na uboreshaji wa huduma ya afya kwa mama na mtoto.
Deiss alieleza hayo alipokuwa akimkaribisha waziri wa Afya wa Zanzibar Juma Duni Haji kuzungumza katika mjadala kuhusu maendeleo yaliyofikiwa katika malengo ya namba nne na tano ya changamoto za Milenia.
Rais huyo alisema Tanzania imekuwa mfano wa kuigwa na ni mdau muhimu katika utekelezaji wa mkakati wa kimataifa kuhusu afya ya mama na mtoto.
“Tanzania ni mdau muhimu katika utekelezaji wa mkakati wa kimataifa kuhusu afya ya mama na mtoto. Rais Jakaya Kikwete ni Mwenyekiti mwenza wa kamisheni ya habari na uwajibikaji katika masuala yanayohusu afya ya mama na mtoto. Tanzania inapiga hatua kubwa na nzuri na imejiwekea malengo na mikakati mbalimbali katika eneo hilo”, alisema Deiss.
Alifahamisha kuwa Tanzania imefanya vizuri katika usambazaji wa huduma za afya, utoaji wa chanjo za kuzuia maradhi mbalimbali kwa wanawake wajawazito na watoto chini ya miaka mitano.
Aidha alipongeza kuwa Tanzania, imejitahidi sana kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano, na inatoa huduma za kinga ya maambukizi ya virusi vinavyosababisha ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto huku ikiendelea na jitihada za kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.
Kwa upande wake akichangia katika mkutano huo, waziri Duni, alisema anajisikia fahari kutamka kwamba Tanzania ilikuwa katika mwelekeo sahihi wa kufikia utekelezaji wa baadhi ya malengo ya maendeleo ya milenia (MDGs).
Waziri aliwaeleza washiriki wa majadiliano hayo, hatua mbalimbali ambazo serikali ya Muungano na ile ya Zanzibar, zimetekeleza malengo namba nne na tano katika utoaji wa huduma za afya ya mama na mtoto, ingawa bado kuna changamoto kadhaa.
Alisema hivi sasa huduma za afya zimesogezwa karibu zaidi na wananchi ili kuwapunguzia wananchi na hasa wanawake mwendo mrefu wa kufuata huduma hizo.
Waziri Duni alisema chanjo za magonjwa mbalimbali zimekuwa zikitolewa kwa wakati na kwa gharama nafuu, huku akielezea kuwa matumizi ya vyandarua vyenye viatilifu vimesaidia sana kupunguza siyo tu vifo vinavyosababishwa na malaria, bali kumetokomeza kabisa ugonjwa huo visiwani Zanzibar.
Aidha alisema kumekuwa na ongezeko la ajira kwa wataalamu wa masuala ya afya, huku akisema ndoa za umri mdogo hasa kwa Tanzania Visiwani bado ni tatizo kubwa.
Awali akifungua majadiliano hayo, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk. Asha-Rose Migiro alirejea wito wake wakizitaka serikali kuwekeza zaidi katika huduma za afya na mama na mtoto.
Mbali na waziri Duni waliokuwa kwenye jopo hilo la mzunguko wa kwanza katika majadiliano hayo ni pamoja na Gilles Richard, Naibu Balozi wa Canada katika Umoja wa Mataifa, Babatunde Osotimehin, Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA. Donna J. Hrinak, Makamu wa Rais kuhusu sera na masuala ya serikali (PepsiCo) na Nyaradzayi Gumbonzvanda, Katibu Mkuu World YWCA.

No comments:

Post a Comment