Friday, 17 June 2011

MISRI KUSAIDIA MAPINDUZI YA KILIMO ZANZIBAR

Misri kusaidia mapinduzi ya kilimo Zanzibar

Na Rajab Mkasaba, Ikulu
MISRI imesema itaendelea kushirikiana na Zanzibar katika mipango yake mbali mbali ya kimaendeleo hasa ufufuaji wa sekta ya kilimo cha umwagiliaji.
Balozi Mdogo wa Misri aliyekuwepo Zanzibar, Walid Mohamed Ismail aliyasema hayo jana alipofanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, Ikulu mjini Zanzibar.
Balozi Ismail alisema kwa kiasi kikubwa Misri inategemea sekta ya kilimo hasa cha umwagiliaji kinachofanywa katika mto Nile, na kwamba uzoefu iliyokuwa nao nchi hiyo utaisaidia kuiinua kilimo Zanzibar na wakulima kuweza kupata tija.
Alisema ana matumaini makubwa kuwa sekta ya kilimo inaweza kuipa msukumo Zanzibar katika kuimarisha uchumi wake pamoja na kuongeza uzalishaji wa chakula.
Aidha, Balozi huyo alimueleza Dk. Shein kuwa mbali na nchi yake kuwa na azma ya kuiunga mkono Zanzibar katika sekta ya kilimo pia, iko tayari kuleta wataalamu kwa ajili ya kuimarisha sekta hiyo ya kilimo na afya.
Balozi huyo alisema nchi yake pia, inaangalia uwezekano mkubwa wa kutoa nafasi za masomo sambamba na kueleza kuwa iko tayari kuwekeza Zanzibar hasa sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.
Kwa upande wake Dk. Shein alisema Zanzibar ina mengi ya kujifunza kutoka Misri kwani nchi hiyo imeweza kupiga hatua katika kuimarisha sekta zake za maendeleo hasa kilimo cha umwagiliaji, ambacho kimekuwa muhimu.
Aidha Dk. Shein alisema ipo haja ya kutilia mkazo zaidi kuwepo kwa kitengo cha tiba ya maradhi ya saratani kwa kutambua kuwa Misri nayo imepiga hatua kubwa katika tiba hiyo.
Alisema lengo la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni kuanzisha kitengo cha kushughulikia maradhi yanayotokana na matatizo ya figo, maradhi ya moyo, maradhi ya saratani na huduma nyengine.
Wakati huo huo Dk.Shein amefanya mazungumzo na Balozi wa Sudan nchini Tanzania AbdelBagi Hamdan Kabeir Ikulu mjini Zanzibar.
Balozi huyo alisema Sudan inathamini uhusiano na ushirikiano uliopo kati yake na Zanzibar na kuahidi utaendelezwa na utaimarishwa zaidi kwa maendeleo ya pande zote mbili.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein pia, alifanya mazungumzo na Balozi wa Uganda Ibrahim Mukiibi ambapo Balozi huyo alisifu uhusiano na ushirikiano kati ya Uganda na Zanzibar.
Viongozi hao kwa pamoja walieleza kuwa amani na usalama ni muhimu sana katika maendeleo ya nchini ambapo pia, Dk. Shein alisifu uhusiano hasa katika sekta ya elimu ambao unahistoria kubwa kati ya nchini mbili hizo ambapo Wazanzibari wengi wamepata elimu katika vyuo vya Uganda kikiwemo Chuo Kikuu cha Makerere.

No comments:

Post a Comment