Monday 13 June 2011

WASIONACHO WASAIDIWE - SALMA KIKWETE

Wasionacho wasaidiwe – Salma Kikwete

Na Anna Nkinda, Maelezo
WANANCHI wenye uwezo wameshauri kujenga mazoea ya kuwasaidia wenzao wanaoishi maisha duni ili nao waweze kupata nafasi ya kufurahia huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo huduma ya elimu na afya.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete alieleza hayo wakati akifungua maonyesho ya mavazi yaliyoandaliwa na Lions Club kwa kushirikiana na wabunifu wa mavazi kwa ajili yakuchangisha fedha za kuzuia upofu na kusaidia kurudisha uwezo wa kuona katika ukumbi wa Kempinski jijini Dar es Salaam.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa juhudi za makusudi zinatakiwa ili utamaduni wa watu kujitolea uweze kujengwa katika maeneo mbalimbali ya jamii kama mashule na katika taasisi ili wanafunzi waweze kujihusisha na huduma za kijamii.
“Ikiwa kila Mtanzania mwenye uwezo atajitolea kusaidia walau mtu mmoja anayetoka katika familia duni hakutakuwa na mtoto ambaye atakosa elimu au mtu atakayekosa tiba kwa kukosa fedha za matibabu,” alisema Mama Kikwete.
Aidha Mwenyekiti huyo wa WAMA alizishauri Taasisi zinazofanya kazi za huduma ya kujitolea ziweze kujitangaza ili watu wenye moyo wa kujitolea waweze kujiunga nao na kuisaidia jamii inayowazunguka.
Kwa upande wake Rais wa Lions Club Dar es Salaam Frank Goyaye alisema kuwa nia ya kuandaa onesho hilo ni kwa ajili ya kuchangisha fedha zitakazotumika kwa ajili ya kuzuia upofu na kusaidia kurudisha uwezo wa kuona kwa wananchi wenye matatizo ya macho na kuihimiza jamii ione umuhimu wa kutunza macho.
Naye kiongozi wa Club hiyo Saruti Shahi alisema kuwa kwa mwaka huu wana programu ya kujenga jengo la wagonjwa wa macho katika mkoa wa Kigoma, jengo ambalo litakuwa nje ya Hospitali ya mkoa na katika jengo hilo kutakuwa na vifaa vilivyokamilika kwa ajili ya kutoa huduma kwa wagonjwa.
Katika harambee hiyo zaidi ya shilingi milioni 15 zilipatikana huku wadau mbalimbali wa maendeleo wakiahidi kuisaidia klabu hiyo kwa hali na mali ili iweze kutimiza malengo yake.

No comments:

Post a Comment