Monday, 13 June 2011

DK. BILAL AWATOA HOFU WATANZANIA WA MAREKANI

Dk. Bilal awatoa hofu Watanzania wa Marekani
Na Mwandishi Maalum, New York
SERIKALI imesisitiza nia yake ya kuhakikisha kwamba zoezi la kukusanya maoni, ushauri na mapendekezo kuhusu mchakato wa kutungwa kwa Katiba mpya linafanyika kwa uwazi na umakini mkubwa.
Hayo yameelezwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohammed Ghalib Bilal wakati alipokuwa akisalimiana na watanzania wanaoishi katika jiji la New York na vitongoji vyake.
Katika mazungumzo yake na watanzania hao yaliyofanyika katika makazi ya Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Makamu wa Rais alisema, ni dhamira ya serikali kuhakikisha si tu inawapa wananchi fursa ya kutoa maoni, ushauri na mapendekezo, lakini kila hoja itakayotolewa itazingatiwa kwa kadri ya uzito wake.
“Tumeanza zoezi hili, ni zoezi ngumu lakini ni zoezi muhimu sana katika kukuza na kudumisha demokrasia yetu. Ni zoezi ambalo linavuta hisia za watu wengi na linafuatiliwa kwa makini sana na wadau mbalimbali wakiwamo wa ndani na nje.” Akasema Makamu wa Rais.
Akasema kuwa hamu ya wadau hao kuufuatilia mchakato huo, inatokana na sababu nyingi lakini kubwa ni kuwa Tanzania bado ni nchi nzuri na inayozingatia utawala wa kidemokrasia.
Akijibu maswali na hoja mbalimbali zilizotolewa na watanzania hao. Yakiwamo maswali kuhusu matatizo ya umeme, mfumuko wa bei hasa kwenye mafuta, uraia wa nchi mbili na fursa za kupata ajira nchini Tanzania.
Katika kuelezea tatizo la umeme, Dk. Bilal alikiri kuwapo kwa tatizo hilo, na akaainisha hatua ambazo serikali imechukua kukabiliana nalo, baadhi ya hatua hizo ni pamoja na kutafuta vyanzo vingine vya umeme kama vile umeme wa upepo, umeme wa gesi asilia na umeme utakao tokana na makaa ya mawe.
Kuhusu bei ya mafuta, Makamu wa Rais alisema kupanda kwa bei ya mafuta ni tatizo la dunia nzima. Hata hivyo akasema kuwa kuna chombo ambacho kimepewa kazi ya kudhibiti bei ya mafuta na ubora wake.
Kuhusu hali ya chakula, Makamu wa Rais alisema kuwa baadhi ya maeneo ya nchi yatakuwa na upungufu mkubwa hasa kwa zao la mpuga kutokana na uhaba wa mvua. Hata hivyo akasema serikali imejiwekea mipango madhubuti ya kuhakikisha kuwa wananchi watakaopungukiwa chakula wanapata chakula kutoka hifadhi ya taifa.
Wakati huo huo, waziri wa Afya kutoka serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Juma Duni Haji amewataka watanzania wanaoishi ughaibuni kuacha kulalamika na kulaumu.
Alikuwa akichangia kujibu maswali kuhusu nini serikali inafanya katika uboreshaji wahuduma za afya .
“Serikali inafanya lile linalowezeka na kila jambo linafanywa kwa wakati wake na kwa kipaumbele chake, matatizo ni mengi na hayawezi kutatuliwa yote kwa wakati mmoja. Lakini nitoe rai yangu, acheni kulalamika na kulaumu, muda wa kulalamika na kulaumiana umeshapita. Kinachotakiwa ni kushirikiana sote katika kujenga nchi yetu” akasisitiza Waziri wa Afya.

No comments:

Post a Comment