Monday, 13 June 2011

SITA MBARONI KWA DAWA ZA KULEVYA.

Sita mbaroni kwa dawa za kulevya

Na Ramadhan Himid, POLISI
KITENGO cha kupambana na dawa za kulevya kilicho chini ya Makao Makuu ya Polisi Zanzibar kimefanikiwa kuwakamata watu sita kwa tuhuma za kupatikana na viwango tofauti vya dawa za kulevya pamoja na majani makavu yanayodhaniwa kuwa ni bangi.
Akithibitisha kukamatwa kwa watu hao Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Zanzibar, Kamishna Msaidizi wa Polisi Muhudi Juma Mshihiri alisema watuhumiwa hao wamekamatwa kufuatia opresheni iliyofanywa na jeshi hilo ili kukomesha biashara ya madawa kulevya nchini.
Aliwataja waliokamatwa katika operesheni hiyo ni Mwanahamis Hija Ali (29) wa Kidongochekundu aliyekamatwa na kete 30 za dawa za kulevya eneo la Malindi Mjini Unguja, Aisha Mohammed Abdalla (27) wa Jang’ombe aliyekamatwa na vidonge 598 vya usingizi aina ya ‘Valium’ Jang’ombe mjini Unguja.
Wengine waliokamatwa ni Rashid Abdalla Haroun (32) wa Magogoni aliyekamatwa na bangi misokoto 13 na bangi iliyosindikwa aina ya ‘charas’ kete 21 huko Ngarugusu wilaya ya Magharibi Unguja, Saleh Mohammed Abdalla (42) wa Miembeni aliyekamatwa na bangi nyongo 28 huko eneo la Kizingo Mjini Unguja, Ali Seif Yahya (25) wa Munduli aliyekamatwa na furushi moja na nyongo 10 za bhangi pamoja na Abdalla Mwenda Makubi (24) wa Mwera aliyekamatwa na nyongo 23 za bhangi eneo la Malindi Unguja.
Nae Mkuu wa Kitengo cha kupambana na dawa ya kulevya Jeshi la Polisi Mrakibu wa Polisi Kheir Mussa aliwataka wananchi kuendelea kutoa taarifa za wahalifu mbali mbali wakiwemo watumiaji wa dawa za kulevya ili kulinusuru taifa na biashara hiyo haramu ambayo huathiri nguvu kazi ya vijana.
Alisema utoaji wa taarifa za wahalifu ni muhimu kwani zimekuwa zikifanikisha wahalifu hao kukamatwa kwa haraka na kufikishwa vyombo vya sheria na kupunguza idadi ya wahalifu mitaani wakiwemo wauzaji, wasambazaji na watumiaji wa dawa za kulevya.
Watuhumiwa wote hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani mara upelelezi utakapokamilika ili kujibu shtuma zinazowakabili.

No comments:

Post a Comment