Friday, 10 June 2011

JUDO ZANZIBAR YAPATA KOCHA MPYA

Judo Zanzibar yapata kocha mpya

Na Mwandishi Wetu
ZANZIBAR imepata kocha mpya wa mchezo wa judo kutoka nchini Japan atakaefanya kazi ya kuwanoa wanajudo wa hapa.
Taarifa zilizotolewa na Chama cha Judo Zanzibar (ZJA), zimefahamisha kuwa, kocha huyo yupo nchini tangu Mei 31, na juzi alikwenda kujitambulisha kwa Waziri wa Habari, Utamkadunbi, Utalii na Michezo Abdilahi Jihad Hassan.
Akizungumza baada ya kumpokea kocha huyo Masahiro Maeda, Waziri wa wizara hiyo Abdilahi Jihad Hassan, alieleza kufurahishwa kwake na ujio wa mwalimu huyo na kusema serikali itatoa ushirikiano wa kutosha ili afanye kazi yake kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ)Hassan Khairallah Tawakal, akimtambulisha kocha huyo alisema, mchezo wa judo Zanzibar umepiga hatua kubwa kutokana na jitihada za chama cha mchezo huo pamoja na wachezaji wake.
Aidha alisema chama hicho kimeonesha uwezo wa pekee miongoni mwa vyama vya michezo mingine, kuiletea sifa nchi kwa kufanya vyema katika mashindano mbalimbali ya ndani na nje wanayoshiriki.
“Judo ni mchezo unaotuletea sifa nyingi hapa Zanzibar , juhudi za viongozi na wachezaji wake zinaonekana wazi na hatuna budi kuwapongeza ili wazidishe jitihada”, alifafanua.
Rais wa Chama cha Judo Zanzibar Tsuyoshi Shimaoka, alimuhakikishia Waziri Jihad kuwa kocha Maeda ana kila sifa inayomfanya aweze kuwapa vijana wa Zanzibar utaalamu wa mchezo huo, na kwamba atakuwepo nchini kwa miaka mitatu kufanya kazi hiyo.
Alisema kuwa kocha huyo ambaye alistaafu kazi katika jeshi la polisi mjini Fukuoka Japan , na kujitosa katika ualimu wa judo, ameshafundisha nchi kadhaa ikiwemo Uturuki, mwaka mmoja, pamoja na Kenya na Nepal ambako kote amefundisha kwa miaka miwili kila nchi.
Maeda ambaye ametokea katika chama cha mchezo huo kilichoko Fukuoka nchini Japan, ana kiwango cha namba saba katika kodokan, ambacho ni cha juu barani Afrika, na tayari ameanza kufundisha klabu ya judo Mlandege tangu tarehe 6, mwezi huu.

No comments:

Post a Comment