Monday, 20 June 2011

MAALIM SEIF ALIELEZA JANGA LA KUPOROMOKA MAADILI.

Maalim Seif alieleza janga la kuporomoka maadili

Asema Zanzibar imepoteza sifa kuwa kitovu cha uislamu
Na Abdi Shamnah
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema vijana wa Kizanzibari wa wakati huu, kwa kiasi kikubwa wanakabiliwa na changamoto ya kuporomoka kwa maadili.
Maalim Seif alisema hayo huko Tomondo, wilaya ya Magharibi Unguja, alipokuwa akizungumza na wazazi, walimu na wanafunzi katika hafla ya ufunguzi wa madrasa ya Qadiriyatul Iman.
Alisema changamoto ya kuporomoka kwa maadili kwa vijana inawezekana endapo masheikh, walimu wa vyuo na madrasa watazingatia wajibu wao katika kuwaandaa vyema watoto na kuwarudisha katika maadili mema.
Maalim Seif alisema kuwa Zanzibar iliokuwa ikisifika sana hapo zamani, kwa kuwa na watu wema, wakarimu na mahala patukufu pa kujifunza elimu ya dini ya kiislamu, imeanza kupoteza haiba na sifa hizo kutokana na na kuporomoka kwa maadili ya watu wake.
Alifahamisha kuwa Zanzibar ilijuilikana katika ukanda wote wa Afrika Mashariki na Kati kama kituo muhimu cha kujifunza uislamu na kuwafanya wanazuoni kutoka nchi mbali mbali (ambao leo ni mashuhuri) kuja kujifunza dini hiyo.
Alisema kutokana na vijana kukosa mafunzo ya dini, wamejikuta wakijiingiza katika matumizi ya dawa ya kulevya, na badala ya kuwa msaada wa taifa wamekuwa mzigo kwa taifa.
Aidha alisema mbali na vijana hao kuwa tatizo katika jamii kutokana na vitendo vyao viovu ikiwemo wizi, lakini pia taifa limepoteza rasilimali yake muhimu katika kuimarisha uchumi wake.
Alifafanua kuwa janga hilo limeziweka familia zote za Wazanzibari katika hali ya mashaka, kwani hakuna hata familia moja inayoweza kujinasibu kuwa iko salama kwa kukosa kijana anaetumia uraibu huo.
Aidha Maalim Seif aliwataka wazazi na walezi wa watoto kuwa na ushirikiano wa karibu na walimu na walielewe jukumu lao katika kuiendeleza madrasa hiyo kwa kutoa michango yao ya hali na mali kwa maslahi yao na watoto wao.
Katika hatua nyingine Makamu wa kwanza wa Rais, aliwakumbusha wazazi na walimu hao juu ya janga la UKIMWI ambalo limekuwa likiwaathiri zaidi vijana na kuanisha kuwa chanzo chake ni zinaa iliotapakaa katika kila pembe ya miji na vijiji.
Alisema njia pekee ya kuondokana na maambukizo ya ugonjwa huo ni kurudi katika misingi ya maadili ya Kizanzibari na kutekeleza kwa vitendo maamrisho ya Mwenyezi Mungu.
Aliwapongeza viongozi na walimu wa Madrasa hiyo kwa juhudi kubwa wanayoichukua kuwaendeleza vijana hao katika elimu za aina zote ikiwemo ile ya dunia na akhera na kuahidi kuchangia shilingi 500,000.
Mapema katika risala yao, wanafunzi wa madrasa hiyo walimweleza Makamu wa Kwanza wa Rais changamoto mbali mbali zinazowakabili, ikiwemo ufinyu wa jengo, vikalio, komputa, printer, mishahara ya walimu, mashirikiano duni kati ya wazazi na walimu pamoja na fedha za kununua kiwanja kipya na gharama za ujenzi wake.
Madrasatul Qadiriatul Iman ilioanzishwa 1993 ina wanafunzi 250, ambapo miongoni mwa masomo yanayofundishwa ni Fikhi,Sira,Tahfidh al kur-an pamoja na kuendesha masomo ya ziada (tuition) kwa wanafunzi wanaokabiliwa na mitihani ya taifa.

No comments:

Post a Comment