Friday 10 June 2011

DK. SHEIN AHUZUNISHWA WAISLAM KUGOMBEA MISIKITI

Dk.Shein ahuzunishwa waislamu kugombea misikiti

Na Rajab Mkasaba, Ikulu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kusikitishwa kwake na tabia iliyoibuka hivi sasa ya Waislamu kutofautiana na kubughudhiana katika mambo ya uongozi wa misikiti.
Dk. Shein aliyasema hayo jana huko Tunduni Wilaya ya Kati Unguja, baada ya kuufungua msikiti wa Tunduni, hafla ambayo ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa dini, vyama na Serikali akiwemo Rais mstaafu Alhaj Dk. Amani Abeid Karume.
Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa jamii ya kiislamu imesahau uongozi wa misikiti kama alivyokuwa akiongoza Mtume Muhamad (S.A.W), ambapo hivi sasa imezuka tabia hiyo ya kutofautiana na kubughudhiana katika uongozi wa misikiti, tabia ambayo haina manufaa katika dini ya Kiislamu.
Alisema kuwa jambo kubwa la msingi ni kutambua kuwa misikiti ni pahala pa ibada na jamii ya kiislamu inapaswa kuheshimu kwa kutambua kuwa ibada inaongoza katika kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu.‘Jamii ya Kiislamu inapaswa kupendana na kuelimishana juu ya mambo yao yote ya kheri’, alisema Dk. Shein.
Aidha, Alhaj Dk. Shein alisema kuwa misikiti ni mahala mwema kwa kufundisha na kusoma Qur-an hivyo aliwataka Waislamu watumie kila fursa kujielimisha na kuendeleza elimu hasa ya Quran kwani elimu kwa Waislamu ni jambo la lazima.
Alhaj Dk. Shein alieleza matumaini yake makubwa kwamba kutokana na historia ya kijiji cha Tunduni kwa Masharifu, msikiti huo pamoja na ibada za sala utumike kama Chuo muhimu cha ufundishaji Quran, hadithi za Bwana Mtume (S.A.W) na Dhikri za kumtukuza MwenyeziMungu.
Alisema kuwa Zanzibar imebahatika kuwa na wajuzi wa Quran na ni vizuri kuwatumia kuendeleza mafunzo yake misikitini na kusisitiza kuwa kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendeleza mfumo wa kuenzi na kuendeleza mafunzo ya Kiislamu katika vyuo vyake viwili vya Kiislamu, pamoja na taasisi za kidini.
Pamoja na hayo, Alhaj Dk. Shein alisema kuwa waislamu wa Tunduni wamekuwa na historia kubwa ya utamaduni wa Dhikri kwa Mwenyezi Mungu na kumuombea kwa Mwenyezi Mungu maghfira na tahfifu mzee Seyyid Noor wa Tunduni ambaye ametumia ujana wake kuongoza dini.
Sambamba na hayo, Alhaj Dk. Shein aliwataka Masheha na Polisi washirikiane na wananchi kudhibiti wizi wa mazao ambao unawavunja moyo wakulima.
Aidha, Dk. Shein aliwataka maafisa wa masoko wasaidie katika kupambana na upelekaji wa mazao machanga sokoni, mengi yao yakiwa yanatokana na wizi na kueleza haja ya kushirikiana katika haya hali ambayo itasaidia kufunga Ramadhani yenye neema kubwa ya vyakula.
Dk. Shein alitoa pongezi na shukurani kwa wote waliohusika na ujenzi wa msikiti huo, zaidi Yakub Osman Sidik na Adil Yakub Sidik na Aila yake pamoja na wananchi wa Shehia ya Tunduni.
Nao wananchi wa Tunduni katika risala yao walieleza kuwa kabla ya ujenzi huo msikiti wao huo ulikuwa haukidhi haja ya wakaazi wa eneo hilo pamoja na wageni wanaowatembelea mara kwa mara.
Walieleza kuwa ujenzi wa msikiti huo mpya ulianza Novemba 11 mwaka jana na kumalizika Aprili 18 mwaka huu baada ya wahisani kuwakubalia kuwapa sadaka hiyo ya kudumu milele yaani ‘Sadakatul-Jaria’.
Wananchi hao wa Tunduni walieleza kuwa misikiti mingi inapokuwa katika hali ya uchakavu na midogo huwa haina migogoro, lakini mara tu inapojengwa na kuwa katika hali nzuri kama ulivyo msikiti wao huo, shetani mbaya huwa anaunyemelea nyemelea.
Walieleza kuwa mara nyingi hujitokeza baadhi ya watu wanaojiona wana elimu ya dini kuliko wengine, jambo ambalo linarejesha nyuma sana juhudi za Waislamu, watu ambao huja na mbinu za kuchomeka mambo ambayo hayaendani na utaratibu wa kidini.
Kutokana na hayo, Wananchi hao wa Tunduni waliahidi kutotokea katyika msikiti wao huo na kueleza kuwa watachukua juhudi zao zote chini ya uongozi wa walimu na mashekhe wao ili msikiti huo uwe mfano mzuri wa kuigwa.
Mapema akitoa hotuba ya sala ya Ijumaa, Katibu wa Mufti, Sheikh Fadhil Soraga aliwataka waumini hao kuepuka tabia ya migogoro ya misikiti kwani aliwaeleza kuwa ni kawaida misikiti inapofikia hatua kama hiyo kujitokeza baadhi ya waumini na kuanza mifarakano.
Alisisitiza kuwa msikiti utumike kwa malengo yake yaliyowekwa kwani iwapo watayafuata hayo mafanikio makubwa yatapatikana.

No comments:

Post a Comment