Monday 13 June 2011

VIJANA MSIOGOPE KUKOPA -- DK. SHEIN

Vijana msiogope kukopa – Dk. Shein

Asema miradi itaongeza ajira, kuondoa utegemezi
Na Mwantanga Ame
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amewataka vijana kutoogopa kuchukua mikopo ya kuanzishia miradi itayoweza kuwapa ajira na kuwaondolea utegemezi.
Dk. Shein alieleza hayo jana alipokuwa akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa jumuiya ya wafugaji huko Fuoni Kibondeni.
Alisema taasisi za kifedha zimekuwa zikitoa mikopo ili iwe chachu kwa vijana kujikusanya pamoja na kuanzisha miradi ambayo itawawezesha kujitegemea kutokana na uzalishaji watakaoufanya na kuondokana na utegemezi.
Alifahamisha kuwa dhamira ya serikali ya Zanzibar ni kuona inaongeza tija katika sekta ya mifugo na ni vyema kwa vijana kutoiogopa mikopo na badala yake wajiandae kuichukua ili waweze kujiajiri na kujitegemea.
Alisema serikali kwa kufahamu matatizo ya mitaji inayowakabili vijana wengi kuweza kuingia katika sekta ya ajira, imeamua kuweka mfuko wa uwezeshaji utaowanufaisha vijana na haipaswi kuiogopa mikopo hiyo.
“Tunachotaka watu wakope na kisha walipe, mimi siipendi ile misemo ya kiswahili inayosema kukopa harusi kulipa matanga, hapana… tukope tulipe”, alisema Dk. Shein.
Alisema kuwa serikali inakusudia kuweka mkakati uliopangwa kutekelezwa mwaka ujao ambao ni kuhakikisha inakuza sekta ya ufugaji na kilimo, kazi ambazo zitaweza kukuza soko la ajira pamoja na maendeleo ya nchi ikizingatiwa kuwa hivi sasa kuna tatizo la ajira kwa wananchi wengi.
Dk. Shein, aliwataka wananchi kujitayarisha kuisikiliza bajeti ijayo kwani itakuja na mabadiliko makubwa na mazuri kwa mwaka ujao wa fedha jinsi ya kukuza sekta ambazo ni muhimu kwa maisha ya wananchi.
Alisema sekta ya ufugaji ni moja ya sehemu muhimu ya uchumi wa Zanzibar, ambapo vijana watapotumia nguvu kazi zao wataweza kufaidika nayo katika kuinua maisha yao na maendeleo nchi pamoja na uchumi wa taifa.
Dk. Shein, alisema ni lazima hivi sasa jamii ya vijana kuona wanabadilika kwa kufuata mfumo wa kidunia kutokana na sehemu kubwa ya vijana wamekuwa wakijiajiri wenywewe ikiwa lengo ni kuona wanapambana na umasikini.
Alisema jambo la msingi ambalo jamii itatakiwa kufanya kuona wanavitumia vyema vyuo vya amali kwani kuwapo kwake vinalenga kuwapatia ujuzi ili waweze kuutumia katika kupambana na umasikini.
Aidha, Dk. Shein, aliitaka jamii wakati wakilitafakari hilo kuzingatia mapambano ya vita dhidi ya UKIMWI yanaendelezwa kutokana na takwimu zake bado kuwa tatizo linaongezeka pamoja na kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya na uharibifu wa mazingira.
Mapema Waziri wa Wizara ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto, Zainab Omar Mohammed, alisema wizara yake inakusudia kuona inawafuata vijana walipo na kuwawezesha ili waweze kujiajiri.
Nae Naibu Katibu Mkuu wa Wizara Hiyo, Mshamu Abdalla Khamis, alisema nia ya Wizara hiyo hivi sasa inadiandaa kufanya sensa ya kuvisajili vikundi na Jumuiya zilizopo nchini.
Mapema wakisoma risala ya Jumuiya hiyo walieleza wanakusudia kukuza sekta ya mifugo ikiwa pamoja na kujipatia ajira kwani sekta hiyo itawawezesha kukuza kiwango cha maisha yao na maendeleo kwa jumla.
Walisema katika mpango wanaokusudia kuanzisha ni juu ya kuihamasisha jamii namna ya kutumia maziwa kutokana na kubaini kuwapo kwa tatizo kubwa la watu kutopenda kunywa maziwa ambapo Jumuiya hiyo inakusudia kuingia katika soko la maskuli.

No comments:

Post a Comment