Monday, 13 June 2011

KIKWETE AALIKWA KUZALIWA SUDAN KUSINI.

Kikwete aalikwa kuzaliwa Sudan Kusini

Na Mwandishi Maalum, Dar
SUDAN Kusini imemualika rasmi Rais Jakaya Mrisho Kikwete kuhudhuria sherehe za kuzaliwa kwa taifa hilo jipya zinazofanyika mjini Juba, Julai 9, mwaka huu, 2011.
Aidha, taifa hilo jipya lina dhamir ya kuchukua kila hatua kuhakikisha kuwa inadumisha amani na utulivu na nchi ya Sudan ambako taifa hilo jipya litameguka.
Mwaliko huo na kauli hiyo ya kudumisha amani vimetolewa Dk. Cirino Hiteng Ofuho, mjumbe Maalum wa Rais wa Sudan Kusini na Makamu wa Rais wa Sudan, Salva Kiir Mayardit. Dk. Ofuho pia ni waziri wa Nchi Ofisi ya Rais wa Sudan Kusini.
Ofuho alimkabidhi Rais Kikwete barua rasmi ya mwaliko kutoka kwa Rais Salva Kiir ikimwomba awe miongoni mwa marais wa nchi mbalimbali duniani wanaotarajiwa kuhudhuria sherehe hizo za kuzaliwa kwa taifa jipya la Sudan Kusini.
Rais Kikwete amekubali mwaliko huo akielezea sherehe za kuzaliwa kwa taifa hilo jipya kama “tukio muhimu na la maana sana” katika historia ya nchi ya Sudan.
Kuzaliwa kwa taifa la Sudan Kusini kunatokana na kura ya maoni ya wananchi wa eneo hilo la Sudan ambao walipiga kura kati ya Januari 9-15, mwaka huu, 2011. Matokeo ya kura hiyo ni kwamba asilimia 98.83 ya wananchi wa Sudan Kusini walipiga.
Kura hiyo ya maoni ilisimamiwa na Baraza Maalum la Wajumbe wa Umoja wa Mataifa wakiongozwa na Rais Mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa.
Kura hiyo ya maoni ilikuwa matokeo ya utekelezaji wa makubalianao ya kuleta amani katika Sudan ya Comprehensive Peace Agreement (CPA) yaliyotiwa saini Januari 9, mwaka 2005, kati ya Serikali ya Sudan na Chama cha Sudan People’s Liberation Movement (SPLM) kwa nia ya kumaliza vita ya pili ya wenyewe kwa wenyewe ambayo inadaiwa kuangamiza maisha ya watu wapatao milioni mbili.
Kuhusu ahadi na dhamira ya Sudan Kusini kudumisha amani na nchi ya Sudan, Dkt. Ofuho amesema kuwa wananchi wa Sudan Kusini wanataka amani siyo kwa sababu ni waoga lakini kwa sababu baada ya miaka mingi ya vita wanahitaji utulivu na kuelekeza nguvu zao katika kuinua maisha yao na kuweka msingi wa vizazi vijavyo.
Dk. Ofuho pia alimueleza Rais Kikwete kuhusu mazungumzo yanayofanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia kati ya Rais Omar El Bashir wa Sudan na Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini kuhusu masuala mbalimbali ambayo hajapatiwa ufumbuzi wakati dunia inasubiri kuzaliwa kwa taifa jipya.
Viongozi hao ambao walianza majadiliano Jumapili, iliyopita walikuwa wanatafuta namna ya kupunguza ushari uliozushwa na tukio la Mei 21, mwaka huu, 2011 wakati yalipozuka mapigano kati ya majeshi ya Sudan na askari wa SPLM ambayo yalisambaa katika eneo la Abyei na kuua watu wengi.
Mara tu baada ya tukio hilo, Rais Kikwete aliwapigia simu Rais Bashir na Rais Salva Kiir akiwataka kutuliza hali hiyo na kutochukua hatua ambazo zingeweza kuzidisha ushari na upotevu wa maisha katika eneo hilo.
Jimbo la Abyei, lililoko mpakani kwa Sudan na Sudan Kusini lina nafasi maalum katika CPA na wakazi wake hawakupiga kura ya maoni mwanzoni mwa mwaka huu kwa sababu pande zote mbili, Sudan na Sudan Kusini, zinalidai jimbo hilo lenye utajiri wa mafuta.

No comments:

Post a Comment