Tuesday 28 June 2011

MAALIM SEIF WANAFUNZI WAHAMASISHWE MASOMO YA SAYANSI

Maalim Seif: Wanafunzi wahamasishwe masomo ya sayansi

Na Abdi Shamnah, Morogoro
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amewataka wahitimu wanaomaliza masomo yao katika Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro, kuwahamasisha wanafunzi kuyapenda masomo ya sayansi ili kukidhi mahitaji ya serikali ya kuwa na wataalamu wa kutosha.
Maalim Seif alitoa changamoto hiyo katika ukumbi wa hoteli ya Bene mjini Morogoro, kwenye hafla iliyoandaliwa na Jumuiya ya ZAMUMSA (Zanzibar University of Muslim Sudents Association), inayowashirikisha wanafunzi kutoka Zanzibar walio katika chuo hicho.
Alisema hatua hiyo inatokana na tatizo la msingi linaloikabili Zanzibar ambapo wahitimu wake wengi ni wale waliojikita katika masomo ya sanaa (art), hali inayoongeza idadi ya wasomi wanaobaki bila ya kuajiriwa, hususan katika sekta ya elimu, baada ya wizara hiyo kusheheni wahitimu wa kada hiyo.
Aliwataka wahitimu hao kulipa uzito unaostahili suala hilo kwa kuzingatia ushindani uliopo mbele yao katika soko la ajira, hususan pale Jumuiya ya Afrika Mashariki itakapoanza kufanyakazi rasmi.
Akizungumzia kushuka kwa kiwango cha elimu Zanzibar, Maalim Seif alisema tatizo hilo linatokana na sababu kadhaa, ikiwemo ya ukosefu wa walimu wenye uwezo wa kutoa elimu bora itakayomuwezesha kijana wa Kizanzibari akimaliza masomo yake kumudu kufanya kazi mahala popote pale Afrika Mashariki.
Alisema serikali ina mipango ya kuzipatia skuli vifaa vyote ikiwemo vitabu na maabara ili kuwawezesha wanafunzi kuendana na wakati uliopo wa Sayansi na Teknolojia.
Alisema ni jambo la kusikitisha kuona skuli za Zanzibar zinashika mkia katika mitihani ya kitaifa kidato cha nne na sita kila mwaka, huku skuli ya SOS pekee ikifanya vizuri kwa kile kinachoonekana kuwepo katika mazingira mazuri.
Katika hatua nyingine Maalim Seif aliwataka wahitimu hao watarajiwa kuwa wazalendo na kurudi nyumbani kulitumikia Taifa badala ya kuendekeza fedha mbele na kwenda nje ya visiwa hivyo kufanyakazi.
Nae Mbunge wa Jimbo la Mkanyageni, Kusini Pemba Mohammed Habibu Mnyaa, aliwataka wahitimu hao kuondokana na dhana potofu kuwa ajira ni ile itokanayo na serikali pekee na badala yake kuangalia umuhimu wa elimu na kuibua njia za kujiajiri.
Mbunge huyo aliitupia lawama Bodi ya Mikopo Tanzania kwa kujenga mazingira yanayowafanya wasichana kujiingiza katika vitendo vya uasharati kutokana na udhaifu wa bodi hiyo, huku serikali ikipaza sauti kupambana na ugonjwa wa UKIMWI.
Katika risala yao wahitimu watarajiwa, walimweleza Makamu wa kwanza wa Rais, juu ya hali ya elimu Zanzibar na mustakbali wake na kuainisha matokeo mabaya kwa wanafunzi wa kidato cha nne na sita.
Wakitolea mfano walisema katika mwaka wa 2011, ni wanafunzi watatu tu ndio waliofanikiwa kupata kiwango cha daraja la kwanza kisiwani Pemba, huku kutoka Unguja kukiwa na wanafunzi sita pekee kutokana maelfu ya watahiniwa wa kidato cha sita.
Jumla ya wahitimu 93 wanatarajiwa kumaliza masomo yao, ikiwa ni muhula wa nne wa chuo hicho, ambapo kati ya wanafunzi hao asilimia 40 ni kutoka Zanzibar, huku wahitimu 50 tayari wakiwa wameshajaza fomu za kuomba ajira katika sekta tofauti Tanzania Bara.
Mahafali hayo yalihudhuriwa na watu mbali mbali, wakiwemo wanafunzi kutoka vyuo vikuu vya MUM, Mzumbe, UDSM, UDOM pamoja Wabunge mbali mbali wakiwemo wale wanaotoka Zanzibar.

No comments:

Post a Comment