Monday, 20 June 2011

RIADHA ZANZIBAR YAZOA DHAHABU NNE UMISETA

Riadha Zanzibar yazoa dhahabu nne Umiseta
Na Donisya Thomas
TIMU ya riadha kutoka Zanzibar, imefanikiwa kunyakua medali nne za dhahabu baada ya wakimbiaji wake kushinda mbio za mita 100 katika mashindano ya Umiseta yanayoendelea wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani.
Aidha timu hiyo imenyakua medali nne za shaba hadi sasa katika mbio za mita 100, ambapo Hamid Hamad anaonekana kufanya vizuri.
Mpasha habari wetu Mussa Abdurabbi aliyeambatana na vijana wa Zanzibar mkoani humo, amesema pia Wazanzibari wameendelea kutamba katika mchezo wa kurusha kisahani kwa wanawake na wanaume.
Aidha kwa upande wa kurusha tufe wanaume, Mkwindi amefanya vizuri huku mwanadada Asha Mshamba nae akifunika kwa upande wa wanawake.
Michuano hiyo inayowashirikisha wanafunzi wa skuli za sekondari Tanzania, imeshuhudia mahaloo wa Zanzibar wakidondoshwa kwa mara ya kwanza katika mpira wa kikapu, walipochapwa na Magharibi vikapu 15-13.
Kwa upande wa wanaume katika kikapu, wakaweza kuwafuta machozi dada zao walipoikandamiza Kanda ya Kati kwa vikapu 66 -35.
Mkuu huyo wa msafara wa timu za Zanzibar, alisema kutokana na ari ya wachezaji wake, ana imani timu hiyo itarejea na vikombe vingi katika mshikemshike huo.

No comments:

Post a Comment