Tuesday, 14 June 2011

SYNOVATE HAIKUVITENDEA HAKI VYOMBO VYA HABAR ZANZIBAR.

Synovate haikuvitendea haki vyombo vya habari vya Zanzibar

Na Ramadhan Makame
UTAFITI kufuatilia ripoti za vyombo vya habari katika uchaguzi mkuu uliopita uliofanywa na kampuni ya Synovate umeelezwa kwamba haukuvitendea haki vyombo vya habari vya Zanzibar kwa kutovielezea uhalisi katika ripoti yao.
Wakichagia ripoti ya Synovate washiriki vyombo hivyo ambao ni wadau wa sekta ya habari na wanasiasa, waliikosoa ripoti hiyo huku wakisema ripoti za vyombo vya Zanzibar hasa vya Umma haikuonekana sawa sawa.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha TADEA, Juma Ali Khatib alisema vyombo vya umma vya Zanzibar vilitoa nafasi bure na sawa kwa kila chama cha siasa lakini utafiti huo haukuonesha.
“Televisheni Zanzibar (TVZ), Redio Zanzibar (STZ) na Gazeti la Zanzibar Leo walitupa nafasi sawa tena tunawashukuru sana nashangaa katika ripoti hii hamna kitu”, alisema mwanasiasa huyo.
Upande mwengine utafiti huo ulibainisha kuwa jambo la kusikitisha ni kwamba vyombo vya habari vilizibania sana sauti za wanawake walioingia katika mchakato wa kuwania nafasi katika majimbo.
“Wanawake hawakupewa nafasi sana ya kuripotiwa sauti za jamii zilifichwa vyombo viliegemea zaidi viongozi kuliko kusikiliza matakwa ya jamii”,alisema Mkurugenzi wa Synovate, Aggrey Oriwo.
Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo ambao umefadhiliwa na shirika la Mipango ya Maendeleo la Umoja wa Mataifa, Mkurugenzi wa Synovate Aggrey Oriwo alisema katika uchunguzi walioufanya vyombo vya habari vya Tanzania vilikibeba chama cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu uliopita, ikilinganishwa na vyama vyengine.
Alisema chama hicho habari zake ziliweza kutangazwa sana na vyombo vyote vya aina tatu ikiwemo magazeti, redio na televisheni zote zikiwa na umma na binafsi.
Akitoa mfano, Oriwo alisema kwa ujumla katika magazeti, Chama hicho kiliibuka na asilimia 48 ya jumla ya habari zote zilizochapishwa huku CHADEMA kikishika nafasi ya pili kwa kujipatia asilimia 24, ambapo CUF ilishika nafasi ya tatu kuwa na asilimia 14.
Alisema hali kama hiyo haikutofautiana sana na taarifa zilizotolewa na
vituo vya televisheni na vituo vya redio zote za binafsi na vya umma.
Kwa upande wake John Mirenyi akiwasilisha mada katika uwasilishwaji wa utafiti huo, alisema vyombo vya habari vina wajibu mkubwa na kuwa makini kuripoti habari zao kwa usahihi, umakini na ueledi bila kupendelea upande wowote katika kipindi cha uchaguzi mkuu.
Aidha alisema wakati wa uchaguzi vyombo hivyo walishindwa kutengeneza ajenda ya kitaifa hali iliyovifanya kugawanyika huku kila chombo kikivutiwa na utashi wake.

No comments:

Post a Comment