Wednesday, 8 June 2011

DK.BILAL AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA MKUTANO WA UKIMWI.

Dk.Bilal aongoza ujumbe wa Tanzania mkutano wa UKIMWI

Na Boniphace Makene, New York
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bilal amekwenda New York nchini Marekani, kuiwakilisha Tanzania katika mkutano wa Umoja wa Mataifa unaozungumzia ugonjwa wa UKIMWI.
Katika mkutano huo ulioandaliwa na UNAIDS, Dk. Bilal anaiongoza timu ya washiriki wa Tanzania ambayo ina wajumuisha asasi za kiraia, uwakilishi wa vijana, wabunge, wadau katika mapambano dhidi ya UKIMWI.
Katika mkutano wake wa kwanza na wawakilishi wa Tanzania kabla ya mkutano huo, Dk. Bilal aliueleza ujumbe wa mkutano huo kutoka Tanzania, kuhakikisha wanafuatilia mkutano huu kwa umakini na kuandika ripoti kwa lugha ya kiswahili.
Alisema lengo la ripoti hizo kuandikwa Kiswahili ni mkutano huo unapokwisha, ripoti hizo ziweze kuwafikia wananchi wa Tanzania kupitia njia zote za mawasiliano na iwe rahisi kufahamika.
Aidha Dk. Bilal alisisitiza umuhimu wa wawakilishi wa Tanzania kuhakikisha kuwa wanautumia mkutano huu vyema na kuwakilisha mawazo ya Watanzania kwa ajili ya kuisaidia Tanzania.
Kwa mujibu wa ratiba ya mkutano huo, Dk. Bilal jana alitarajiwa kuwasilisha hotuba iliyofafanua kuhusu nafasi ya Tanzania katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI, ambayo ilielezea jinsi Tanzania na wananchi wanavyojitahidi katika kuhakikisha kasi ya maambukizi mapya inapunguzwa.
Aidha akiwa jijini New York, Dk. Bilal anatarajiwa kukutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, ambapo mazungumzo yao yanatarajiwa kuzungumzia nafasi ya Umoja wa Mataifa katika mapambanao dhidi ya UKIMWI.
Kwa mujibu wa Ratiba ya Makamu wa Rais, atakutana na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Dk. Asha Rose Migiro siku ya mwisho ya mkutano, huku pia akitarajia kuwa na mahojiano na vyombo kadhaa vya kimataifa ili kufafanua nafasi ya Tanzania katika mapambano dhidi ya UKIMWI.
Ratiba hiyo pia inaonyesha kuwa Makamu wa Rais atafanya mikutano kadhaa iliyoandaliwa na nchi za Marekani na Uingereza ambao ni wadau wakubwa katika kuisaidia Tanzania katika mikakati ya kupambana na UKIMWI.
Makamu wa Rais ameambatana na mkewe Zakia Bilal ambaye naye ataungana na wake wa viongozi wa nchi mbalimbali katika mijadala ya nafasi yao katika kukabiliana na janga la UKIMWI.
Viongozi wengine waliokuwemo katika zaira hiyo ni pamoja na Waziri wa Afya Zanzibar, Juma Duni Haji, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Mahadhi Juma Maalim, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Fatma Fereji na viongozi wengine wa wizara ya Afya.

No comments:

Post a Comment