Wednesday 8 June 2011

KILIMO CHA MPUNGA KUFANYIWA MAGEUZI.

Kilimo cha mpunga kufanyiwa mageuzi

Na Nafisa Madai, Maelezo
WAZIRI wa Kilimo na Maliasili, Mansoor Yusuf Himid, amesema mipango ya serikali ni kuhakikisha hadi mwaka 2015 hekta 6,000 ziwe zinalimwa na kuzalisha mpunga ili kupunguza uagizaji wa mchele kutona nchi za nje.
Mansoor alieleza hayo jana wizarani kwake Darajani mjini hapa, alipokuwa na mazungumzo na Balozi wa Indonesia nchini Tanzania, Yudhistirano Sungad.
Alisema serikali itahakikisha inawawezesha wakulima wa visiwani ili kulima hekta hizo, hali itakayowezesha wananchi kujitosheleza kwa chakula na kupunguza uagizaji wa mchele kutona nje.
Alifahamisha kuwa hivi sasa kiasi cha shilingi milioni 45 zinatumikwa kwa mwaka kuagizia mchele kutoka nje, ambapo mahitaji ya wananchi ya mchele kwa mwaka ikiwa ni tani 80.
Waziri huyo alisema hali ya uzalishaji mpunga Zanzibar hivi sasa haiwiani na matumizi ya mchele ambapo wakulima nchini kwa mwaka huzalisha tani 16, kiasi ambacho hakikidhi hata robo ya mahitaji ya wananchi wa Zanzibar.
Akitaja sababu zinazokwaza wakulima kutolima kwa wingi mpunga visiwani hapa ni ukosefu wa vitendeakazi, mbinu duni na ukosefu wa pembejeo za mbole.
Aidha waziri huyo aliishukuru serikali ya Indonesia kwa uamuzi wake kuisaidia Zanzibar katika sekta ya kilimo husani kilimo cha mpunga ambapo imekuwa kilio cha wakulima wa zao hilo.
Balozi wa Indonesia nchini Tanzania, alisema serikali yake imeleta wataalamu wawili nchini ili kusaidia taaluma kwa wakulima na kuweza kuzalisha mpunga kwa wingi na wenye viwango.
Aidha alisema wataalamu hao wataweza kutoa elimu ya matumizi ya elimu ya mbolea isiyo na kemikali ili kuilinda afya ya mlaji pamoja na uharibifu wa ardhi.
Balozi Yudhistirano alisema Indonesia na Zanzibar zimekuwa na urafiki wa muda mrefu, hivyo ni muhimu kutumia utaalamu iliyonao kusaidia kuinua kilimo hapa visiwani.
Mazungumo baina ya waziri Mansoor na Balozi Yudhistirano yamekuja kufuatia mazungumzo ya awali yaliyofanyika miezi miwili iliyopita, na leo hii balozi anatarajiwa kutembelea mabonde yanayotumika kwa kilimo cha mpunga.

No comments:

Post a Comment