Wednesday 8 June 2011

WIZARA YA AFYA YAKANUSHA BAJETI YAKE KUKWAMA.

Wizara ya Afya yakanusha bajeti yake kukwama

Na Mwanajuma Abdi
WIZARA ya Afya Zanzibar imetoa ufafanuzi juu ya taarifa iliyotolewa na gazeti moja la kila siku la Dar es Salaam kuhusiana na madai ya bajeti ya Wizara hiyo kukwamishwa na Kamati ya Baraza la Wawakilishi.
Wizara hiyo imetoa wiki moja kuombwa radhi na mwandishi wa habari wa gazeti hilo aliyeko Zanzibar kwa kuandika taarifa za kupotosha umma.
Akizungumza na waandishi wa habari, katika Ofisi za Wizara hiyo, Mkurugenzi wa Uendeshaji na Utumishi, Juma Rajab alisema wametoa wiki moja kuombwa radhi kupitia gazeti hilo la si hivyo watamfikisha katika vyombo vya sheria.
Alisema gazeti hilo la jana, kichwa cha habari kimesema Bajeti ya Wizara ya Afya Zanzibar yakwama, habari hiyo alisisitiza sio ya kweli kwani bajeti bado haijasomwa na kamati ya Baraza la Wawakilishi haina uwezo wa kuzuia, ambapo kazi yake kubwa ni kupitisha vifungu na masuala mengine.
Alieleza uwezo wa kukwamisha bajeti ni wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanapokuwa ndani ya ukumbi huo na sio kamati.
Mkurugenzi Juma Rajab alisema kilichojitokeza jana, hadi kikao cha kamati kuahirishwa ni kutokana na baadhi ya wajumbe kutohudhuria, ambapo aliwaomba radhi wajumbe wa kamati BLW inayoshughulikia masuala ya Ustawi wa Jamii, Wanawake na Watoto.
“Gazeti limeandika kwamba, bajeti imekwama kupitishwa kwa kukosa kasma ya manunuzi ya dawa na Mkemia Mkuu kutengezwa shilingi milioni mbili tu kwa ajili ya mafunzo, kamati pia imeona si busara kwa wizara hiyo kutenga shilingi milioni 600 kwa ajili ya semina za watendaji wakuu, sambamba na Wizara ya Agya inatarajiwa kutumia zaidi ya shilingi bilioni nne katika mwaka ujao wa fedha”.
Mkurugenzi Sera, Mipango na Utafiti, Abdul-latif Khatib Haji alifafanua kuwa, taarifa hiyo sio sahihi kwani Wizara hiyo inatarajia kutumia zaidi ya shilingi Bilioni 10 katika bajeti yake mwaka ujao wa fedha na sio shilingi bilioni nne.
Aidha aliongeza kusema kwamba, Serikali imetenga fedha zaidi ya shilingi milioni 749 kwa ajili ya manunuzi ya dawa na vifaa ambazo zitaingizwa katika kasma ya Mfamansia Mkuu, ambapo hatua hiyo ni kubwa ukilinganishwa na huko nyuma kulikuwa na fungu dogo la manunuzi ya dawa na fedha zilizobakia zilikuwa zinategemewa kutoka kwa wahisani.
Hata hivyo, alikanusha vikali kwamba Wizara hiyo imetenga shilingi milioni 600 kwa ajili ya semina za watendaji, ambapo alisema kiwango hicho cha fedha ni kikubwa kwa kutumia kwa mafunzo wakati kuna mambo mengi yanahitajika kufanywa.
Mkurugenzi huyo alisema Ofisi ya Mkemia Mkuu imetengewa zaidi ya shilingi milioni 47 katika mwaka wa fedha ujao na sio shilingi milioni mbili, ambapo bajeti bado haijawasilishwa na kwa sasa Serikali imo katika mchakato wa kupitia bajeti za Serikali katika Wizara mbali mbali kupitia kamati za wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

No comments:

Post a Comment