Askofu ataka ‘mafisadi’ wachukuliwe hatua
• Asema Serikali zifikie matumaini ya wananchi
• Haoni sababu kuwepo maskini Tanzania
Na Mwanajuma Abdi
ASKOFU Augustine Ndeliakyama Shao wa kanisa la Roman Catholic Zanzibar, amesema watanzania wanalia na kuvunjika moyo na ubadhirifu na mishahara hewa kwa baadhi ya viongozi nchini hali inayosababisha kukosekana kwa nyenzo maskulini, vyuo na uhaba wa dawa hospitalini.
Hayo aliyasema jana, katika hotuba aliyoitoa katika kanisa la Minara miwili Shangani mjini Unguja kwa waumini wa dini ya kikristo ikiwa ni ujumbe wa Pasaka 2011 ‘mwanga unaoleta uhuru kwa mwanadamu aliyekuwa kwenye giza la maovu’.
Alisema watanzania wamekata tamaa na nchi yao kutokana kusikia ubadhirifu mkubwa na upoteaji wa fedha za mishahara hewa inayofanywa na baadhi ya viongozi waliopo katika madaraka nchini huku huduma muhimu zikikosekana katika hospitali na maskulini.
“Wakati watanzania wakitarajia mengi mazuri kutoka kwa Serikali zao lakini wanapata ripoti za ubadhirifu wa baadhi ya viongozi katika Wizara, Mikoa, wilaya na taasisi mbali mbali wakifaidika kwa mishahara hewa na wengine kushindwa kutoa ankara za matumizi, wakati huku mahospitali yakiwa na uhaba wa dawa muhimu, shule na vyuo vikiwa havina nyenzo muhimu za kufundishia”, alisema Askofu Shao.
Alisema hayo hayawezi kufanyika kama hakuna utawala wa sheria, watanzania wanaotegemea huduma nzuri kwa gharama ya kodi zao hawajasikia hatua zinazochukuliwa au zilizochukuliwa dhidi ya ubadhirifu huo.
Alieleza ufufuko wa kristu ni agizo la kutafuta sababu za wengi kuwa masikini na wachache kuwa matajiri wa kupindukia katika nchi tajiri kama Tanzania, ambapo aligusia popote pale penye mateso njaa na umasikini unatokana na uvunjwaji wa haki za binadamu.
Askofu Shao alitoa wito kwa viongozi wa jamii kuangalia upya sheria za ardhi, madini na biashara katika kukuza uchumi kwa watu wote bila ya kuweka tabaka.
Aliwaeleza waumini hao kwamba, Serikali inakimbizana na wamachinga na wakulima wadogo wadogo wanaobeba mazao na bidhaa zao kichwani na migongoni kwa ajili ya kutafuta riski kwa kuwabebesha kodi kubwa huku ikiendeleza misamaha kwa wawekezaji na wafanyabiashara wakubwa, ambao wangalisaidia kunyanyua uchumi badala ya kutwishwa mzigo wadogo.
“Kodi ya mfanyabiashara anayeingiza kontena 50, muwekezaji katika hoteli au madini hawa wote wakilipa kodi uhakika kwa kipindi kifupi nchi yetu itafikia malengo ya maendeleo”, alisisitiza.
Aidha alisema, kwa miezi sita hivi kumekuwepo kwa Serikali mpya, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa na ile ya Serikali ya Muungano Tanzania, ambapo watanzania walikuwa na matarajio makubwa ya mabadiliko hayo yataleta matumaini.
Aliongeza kusema kwamba, ni mapema mno kutoa tathmini lakini kwa kusoma alama na matukio machache, wengi wao hawajaona nia ya dhati ya kutaka mabadiliko na utayari wa baadhi ya viongozi kupokea mawazo na changamoto za wengine kwa kuona nguvu mpya, ubunifu mpya wa rika mbali mbali, vipaji tofauti na itikadi mbali mbali katika Wizara, Wilaya, Mikoa na Taasisi za Serikali.
Hata hivyo, alitoa wito kwa waumini kwamba agizo la ufufuko ni kuwaonesha watu kwa uhakika wote kwamba kristu ni Mkombozi wa dunia ameshinda maovu yote, amejenga matumaini na kwamba wote wana haki ya uhai wenye furaha.
Jana wakristo duniani kote walisherehekea maadhimisho ya kufufuka kwa kiongozi wao Yesu Kristo, baada ya kufariki siku ya Ijumaa Kuu.
Sunday, 24 April 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment