Monday 11 April 2011

BABU KIKOMBE AIBUKA ZANZIBAR

Babu kikombe aibuka Zanzibar

Mwantanga Ame

HATIMAYE dawa ya asili yenye kuaminika kutibu maradhi sugu baada ya kuibuka kutolewa katika mikoa kadhaa ya Tanzania bara huku watu kufurika kuinywa, mkaazi mmoja wa Fuoni Zanzibar naye amejitangaza kutoa dawa hiyo.

Mtoa dawa huyo asili aliyejitambulisha kwa jina la Rashid Msigwa kutoka Kigoma Tanzania, amedai kuvumbua dawa aina ya ‘4A9 Medicine’ inayotibu magonjwa sugu ikiwemo UKIMWI.

Alisema dawa yake imeanza kutumika zaidi ya mikoa 11 ya Tanzania Bara ikiwemo Kigoma, Arusha Mwanza, Iringa, Dar es Salaam na mikoa mingine ambapo watu kadhaa wenye maradhi sugu waliotumia dawa yake wamepona.

Msigwa alisema matumizi ya dawa yake mgonjwa hulazimika kutumia kichupa kimoja au viwili hadi kupona kabisa, huku akikataa kata kata kutaja aina ya miti anayotumia katika kuitengeneza dawa hiyo.

Alisikitishwa kukosekana ushirikiano kwa taasisi za juu za Afya ikiwemo Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ya Jamhuri ya Muungano Tanzania, hali iliyochangia kushindwa kutambuliwa dawa hiyo.

Alisema hadi sasa ameweza kutibu zaidi ya wagonjwa wapatao 800 hapa Zanzibar katika kipindi kifupi alichokaa na amekuwa akipokea wagonjwa wengi wanaosumbuliwa na maradhi mbali mbali ikiwemo maradhi ya kisukari, UKIMWI na magonjwa mengine ya akina mama.

Akitaja matumizi ya dawa zake Mganga huyo alisema kazi ya dawa hiyo ni kusukuma damu mwilini, kuongeza madini ya chuma, kuongeza kinga katika mwili na kujikinga na maradhi mbali mbali.

Msigwa alisema ameigundua dawa hiyo miaka mingi ambapo kwa zaidi ya miaka 13, inafanya kazi ya kuwatibu wagonjwa mbalimbali ndani na nje ya nchi, dawa ambayo iligunduliwa na mama yake mzazi aliyekwisha fariki.

“Tatizo lililopo ni kati ya wataalamu wa kizungu na sisi waganga wa tiba asili, waganga wa dawa hizi za mitishamba tunawekewa kikwazo wakidai wanaifanyia utafiti jambo ambalo linachelewesha dhana nzima ya utoaji tiba kwa wagonjwa”, alisema.

Alifahamisha kuwa Baraza la Tiba Asili la Zanzibar na Bodi ya Chakula Dawa na Vipodozi, wanaitambua dawa hiyo jambo ambalo limerahisisha wagonjwa wengi kufika kwake kutibiwa.

“Mimi sharti langu ni kwamba kabla hujatumia dawa zangu basi hutaka lazima ukapime afya yako ili ukitumia nijue ni virusi ulivyonavyo mwilini na baada ya kumaliza kutumia dozi yangu pia hutaka wende ukapime vile vile ili tujue waliobaki na kama wameshamalizika”, alisisitiza.

Akifafanua kwamba baadhi ya watu wenye virusi vya UKIMWI kwa watu wenye CD4 kiwango cha 427 na baada ya wiki mbili mgonjwa huyo huyo CD4 zake ziliongezeka na kufikia 613.

“Mimi dawa yangu inayo uwezo wa kuongeza CD4 kwa muda wa wiki moja tofauti na zile za kupunguza makali ya virusi za ARVs na kabla ya kumpa mgonjwa dawa nataka kwanza akapime na aje na vipimo vyake ndipo aweze kutumia daa hizi”. alisema Msigwa.

Akitoa ushuhuda mmoja ya waliokuwa wagonjwa Jaffar Masale alidai alikuwa na UKIMWI lakini baada ya kutumia dawa hiyo amepona kabisa kwa mujibu wa vipimo alivyopewa hospitali mbali mbali alizokwenda kupima.

“Niseme nilikuwa katika hali mbaya baada kubaini nimeathirika UKIMWI, nilikuwa naharisha na ngozi yangu yote kuharibika lakini baada ya kutumia dawa hiyo sasa nipo salama na ninaweza kufanya kazi zangu vizuri na nashukuru kwamba hivi sasa nimepata nguvu ya kufanya kazi”, alisema Masale.

Shuhuda mwengine ni mhadhiri wa Chuo Kikuu, Abdulkadir Mohammed alisema alikuwa akisumbuliwa na malaria sugu ambayo kwa miezi kadhaa alikuwa akitumia dawa bila ya mafanikio lakini baada ya kutumia dawa za Msigwa amepona.

Msigwa alitoa ombi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupatikana kwa mashine ya kujuwa kiwango cha virusi katika damu ya binaadamu inayojulikanana kwa jina la ‘Viral load’ ili wananchi wapate kwenda kupima afya zao kupitia kipimo hicho.

Nchini Tanzania kumeibuka na kuchipua watoa tiba asili kwenye mikoa kadhaa ambao wanadai dawa zinatibu maradhi sugu kama vile UKIMWI, shindikizo la damu, sukari na kadhalika.

No comments:

Post a Comment