Tuesday, 26 April 2011

WAVUVI WAPEWE ELIMU KUEPUKA UHARIBIFU WA MAZINGIRA

Wavuvi wapewe elimu kuepuka uharibifu wa mazingira

Na Halima Abdalla
JUMUIA ya maendeleo ya jamii na uhifadhi wa Mazingira Zanzibar (CODECOZ), imetakiwa kuelimisha wavuvi kuhusiana na zana bora za kuvulia ambazo haziharibu mazingira ya baharini ikiwemo matumbawe.
Mjumbe wa bodi ya udhamini wa CODECOZ, Dk.Nerrman Jidawi alieleza hayo alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa jumuia hiyo unaohusiana na mapato na matumizi yaliyotumika kwa mwaka uliopita na yatakayotumika kwa mwaka huu uliofanyika katika ukumbi wa Takwimu Mwanakwerekwe mjini hapa.
Aliwataka kuendelea kuelimisha jamii umuhimu wa uhifadhi na utunzaji wa mazingira sambamba na kuelimisha wavuvi kuhusu umuhimu wa matumbawe ambayo ni kivutio kikubwa cha utalii na ni sehemu ya mazalio ya samaki, hivyo yanahitaji kutunzwa ili yaweze kuongeza pato la Taifa.
Aidha aliwataka wanachama wa CODECOZ, kushirikiana na serikali katika kudhibiti suala zima la uingiaji wa mifuko ya plastiki ambayo inaendelea kuzagaa nchini.
Dk. Jidawi alisema suala la kuzagaa kwa mifuko ya plastiki limeenea kila sehemu kwa Zanzibar hasa mifuko inayotokana na mauzo ya bidhaa mbalimbali ambayo imetapakaa mjini pamoja na mifuko inayotumiwa kwa ajili ya kununulia bidhaa.
Akizungumza katika mkutano huo Mwenyekiti wa Jumuia hiyo Hamza Rijaal, alisema jumuia yao inakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo ukosefu wa ofisi ya kudumu, ukosefu wa fedha za kuweza kuajiri watendaji wa kudumu pamoja idadi ndogo wa wanachama.
Katika mkutano huo wa mwaka wa jumuia ya CODECOZ kuhusiana na mapato na matumizi yaliotumika kwa mwaka uliopita ambao umeishia na Disemba 2010, umeweza kutumia shilingi milioni 32,264,500 mapato ambayo yanatoka kwa wafadhili pamoja ada za wanachama na michango ya wanachama.
Aidha kwa mwaka huu kuanzia mwezi Januari 2011 hadi Disemba 2011 Jumuia hiyo inategemea kutumia milioni 46,569,000 katika kufanikisha shughuli zao ambazo zitatokana na vyanzo vyao vya mapato.
Jumuia ya CODECOZ imeanzishwa mwaka 1996 na ina wanachama 49.

No comments:

Post a Comment