Thursday, 28 April 2011

BIHINDI AITAKA UNICEF KUISAIDIA ZANZIBAR.

Bihindi aitaka UNICEF kuisaidia Zanzibar

Na Zuwena Amour, WHUUM
NAIBU waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Bihindi Hamad Khamis ameliomba shirika la Umoja wa Mataifa lenye kushughulikia watoto (UNICEF), kuendelea kuisaidia Zanzibar.
Bihindi alieleza hayo jana alipokuwa akizungumza na ujumbe wa maofisa wa Shirika hilo waliofika ofisini kwake Kikwajuni mjini hapa.
Alisema UNICEF ni Shirika lenye miradi mbalimbali ya kijamii ambayo kwa kiasi kikubwa inaweza kuwanufaisha wananchi wa Zanzibar.
Aidha Naibu huyo alilipongeza shirika hilo kwa ushirikiano wake na Zanzibar sambamba na miradi ya kijamii inayoisaidia Zanzibar ambayo imekuwa na faida kubwa kwa wananchi.
“Naomba ushirikiano kati yetu uzidi kuimarika kwa faida ya wananchi”, alisema Naibu huyo.
Bihindi pia alitumia nafasi hiyo kuliomba shirika hilo kutoa vifaa mbali mbali pamoja na mafunzo kwa taasisi za habari za Zanzibar.
Nao kwa upande wao maofisa hao wa UNICEF, Ruth Leano na Bisa Cameron walimhakikishia waziri huyo kuwa shirika hilo litaendelea kuisaidia Zanzibar.
Walisema shirika hilo linakusudia kuanzisha programu katika vyombo vya habari ambayo itaelezea athari za mimba za utotoni, elimu ya UKIMWI, matatizo ya wanawake pamoja na udhalilishaji.
Katika ziara hiyo pia maofisa hao waliangalia miradi ambayo wameisaidia wizara hiyo likiwemo gari la sinema ambalo limekuwa likitumika kutolea elimu kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment