Thursday 28 April 2011

UDHAIFU, UBINAFSI SUMU YA MUUNGANO -RAZA

Udhaifu, ubinafsi sumu ya Muungano - Raza

Na Ramadhan Makame
MFANYABIASHARA maarufu visiwani Zanzibar Mohammed Raza, amesema matatizo yanayojitokeza kwenye mchakato wa katiba mpya na masuala ya Muungano yanatokana na udhaifu wa watendaji wanaojali maslahi yao binafsi na kuliyumbisha taifa.
Raza alieleza hayo jana katika hoteli Grand Palace, iliyopo Malindi mjini hapa alipokuwa akitoa tathmini aliyoombwa kuitoa juu ya mchakato wa katiba na masuala ya Muungano.
Alisema watendaji wa ngazi za kati ndio wababaishaji wa mambo, ambapo wamekuwa na unafiki, tamaa, uchu na uroho wa madaraka hali inayosababisha kujitokeza kwa matatizo.
“Wakati mwengine tumekuwa tukiwalaumu Watazania bara mengine yanasababishwa na watendaji wetu kwa kuwa wanafiki na wasiojali maslahi ya wananchi”, alisema Raza.
Alisema viongozi wakuu wa nchi wana nia njema ya kuliongoza taifa hili kwa amani na utulivu, lakini uchu wa madaraka na unafiki wa watendaji umekuwa ukiliyumbisha taifa kwa kujali maslahi yao zaidi ya wananchi.
“Wananchi wa Zanzibar ni watulivu, wapenda amani wanaopenda kushirikiana na wasiopenda ugomvi, lakini matatizo yapo kwa hawa wasaidizi wa viongozi wa juu”,alisema Raza.
Raza alisema suala lililo mbele ya wananchi wa Zanzibar ni kusimama pamoja na kujenga hoja wakiongozwa na hadidu rejea ‘terms of reference’ kuwa Zanzibar nchi iliyokuwa huru kabla ya kuungana.
“Hili lazima tuliweke wazi na nimelisema kwa zaidi ya miaka 20, na wabunge wetu walielewe, Zanzibar ilikuwa nchi kamili kabla ya kuungana na wala tusikubali kuburuzwa”, alisema.
Alisema wakati wa wananchi kuwekewa ‘menu’ na kikundi cha watu 20 na kuambiwa haya ndio maamuzi umekwisha, bali washirikishwe kikamilifu katika kila lenye maslahi ya kujenga nchi.
Alisema ufike wakati Watanganyika na Wazanzibari wavumiliane na kila mmoja asione mzigo kwa mwenziwe na kusisitiza kuwa aandamwe mwenye kutaka kuvunja Muungano.
Alisema hata hivyo wakati utakapofika wa kijadili katiba wananchi waruhusiwe aina ya Muungano wanaoutaka na serikali wanazozitaka.
Raza amelezimika kuitisha mkutano huo akidai kuwa ameombwa kufanya hivyo na wananchi wa Zanzibar na hiyo imekuwa kawaida yake kila yanapotokezea masuala yanayolihusu taifa.

No comments:

Post a Comment