Thursday, 28 April 2011

MAGUFULI AINGIA HOMA UFISADI KIGAMBONI.

Magufuli aingia homa ufisadi Kigamboni

Na Kunze Mswanyama, Dar
WAZIRI wa Ujenzi Dk. John Pombe Magufuli, amevunja ukimya na kuwanyooshea kidole wakala wa serikali wa ufundi na umeme nchini (TEMESA), kukithiri ufisadi na hasa kwenye kivuko cha Magogoni kinachosimamia vivuko vya kwenda na kurudi Kigamboni.
Waziri Magufuli, alieleza hayo alipokuwa akizindua bodi mbili zilizo chini ya wizara yake za wakala wa Majengo na Wakala wa Ufundi na Umeme jijini Dar es salaam, jana kufuatia kuziteua bodi hizo hivi karibuni.
"Boti kubwa yenye uwezo wa kupakia watu zaidi ya 2,000 na magari 60 na ina injini nne nilipokwenda niligundua kuwa zinazofanya kazi ni injini mbili, lakini mafuta yanayoagizwa ni injini zote nne, huu ni ufisadi mkubwa, inaniuma kweli",alisema Dk. Magufuli.
Waziri huyo alisema hayo aliyashuhudia alipofanya ziara ya kushtukiza katika kivuko cha Magogoni na hatimaye kubaini ufisadi ambapo alivaa kanzu na kofia kubwa "pama" hali iliyofanywa watumishi kutomgundua.
“Haiwezekani kivuko hicho kuingiza mapato ya shilingi milioni 7.5 kwa siku ilhali ukaguzi uliofanywa ulionyesha kuwa kuna kila sababu ya kuingiza zaidi ya milioni 10, siku moja nitafanya ziara mimi na Mwakyembe tuone kama hatutapata kiasi hicho",alisema.
Alisema ameamua kuingiza wanajeshi katika bodi hiyo ili kurudisha nidhamu ndani ya chombo hicho kilichoanza kupoteza mwelekeo siku za hivi karibuni.
Wakala huyo ambaye pia aliwahi kulalamikiwa sana na Naibu waziri wa Ujenzi Dk.Harison Mwakyembe kwa ufisadi,umekabidhiwa wanajeshi wawili wenye vyeo vya Ujenerali ili kuongeza uwajibikaji zaidi na hivyo kuiingizia serikali mabilioni ambayo kwa sasa kwa kiasi kikubwa yanaishia kwenye mifuko ya mafisadi.
Aidha, Magufuli aliwataka wajumbe hao ambao watakuwa madarakani kwa muda wa miaka mitano na wakiongozwa na Pro.Idris Mshoro ambaye ni Makamu Mkuu wa chuo Kikuu cha Ardhi kufanya kazi kwa bidi ili kuiwezesha wakala huyo kuwa na uwezo wa kujihudumia na hivyo kuboresha mishahara ya watumishi wao.
Pia Magufuli alisema anaamini kuwa kwa kutumia bodi hiyo mpya ya ushauri sasa watahakiksha kuwa magari, mitambo na mashine mbalimbali ya serikali na hata ya watu binafsi inapelekwa kutengenezwa na kufanyiwa marekebisho hapo na hiyo itarudisha heshima yao ilyoanza kushuka tofauti na ilivyokuwa ni Idara ya Ujenzi.
Aidha, alihoji kwa nini magari na mitambo ya serikali ipelekwe kutengenezwa kwenye gereji za "chini ya mwembe" wakati TEMESA wapo nchi nzima na ambapo alitaka kujua kama mafundi wao (TEMESA) hawana ujuzi au wanaiba vifaa kiasi cha kuwakatisha tamaa wateja.
Kwa upande mwingine Magufuli aliisifu Wakala wa Majengo kwa kuwa kupitia kwao serikali imewezesha kujengwa kwa nyumba zaidi ya 1025 ambazo zinaweza kuuzwa kwa watumishi au kuwa za kuishi watumishi waliopo kazini.

No comments:

Post a Comment