Serikali kugawa gesi bure
Ni kusaidia uhifadhi mazingira
Na Mwantanga Ame
SERIKALI imeandaa mpango wa kuwapatia wananchi gesi bure kwa matumizi ya nyumbani ikiwa ni hatua ya kukabiliana na matumizi mabaya ya nishati za raslimali ya misitu.
Mbali ya hatua ya serikali kugawa gesi bure pia inakusudia kuhamasisha matumizi ya majiko ya gesi sambamba na kupunguza bei ya majiko hayo ili wananchi wengi wamudu gharama za kuyanunua.
Mpango huo unatekelezwa na serikali kupitia mradi maalum (HIMA) unaofadhiliwa na serikali ya Norway, baada ya kuipatia Zanzibar chini ya Wizara ya Kilimo na Mali Asili, dola za Kimarekani milioni 4/= na utatekelezwa kwa kipindi cha miaka minne.
Akizungumza na waandishi wa Habari, Naibu Katibu Mkuu Mali Asili, Dk. Bakari Asseid, alisema mradi huo tangu kuanza mwezi Julai mwaka uliopita tayari umeshawafaidisha watu 1,000 wa Zanzibar, ambao wamekuwa wakitumia gesi kwa matumizi ya nyumbani na kuachana na matumizi ya kuni.
Alisema uamuzi wa serikali kutoa gesi hiyo bure ikiwa ni hatua itayomuwezesha mwananchi kuacha kutumia nishati za misitu huku akiweza kusaidia kulinda mazingira ya Zanzibar.
Alisema katika mradi huo, unahusisha watumiaji wa majiko ya gesi katika maeneo ya majumbani, mahotelini, bekari, dahalia na vikosi vya Ulinzi na Usalama.
Alisema Wizara hiyo imeamua kuanzisha mradi huo kwa lengo la kuwahasisha wananchi ili waweze kutumia majiko ya gesi na kuweza kupunguza kiwango kikubwa cha nishati ya misitu kinachoendelea kuvunwa kwa matumizi ya nishati.
Alisema hivi sasa Zanzibar kwa mwaka kunavunwa hekta 600 za misitu hupotea kwa Unguja na Pemba huku kukiwa na hekta 450 zinazopandwa ikiwa ni sawa na asilimia 50 ikiwa ni uwiano mdogo wa uvunwaji na upandwaji.
Kutokana na hali hiyo Dk. Aseeid, alisema mradi wa HIMA kuja kwake utaweza kupunguza tatizo la uharifu wa mazingira unaotokana na ukatwaji wa miti na kuwapa fursa wananchi kuendeleza kulinda na kuhifadhi mazingira kwa faina ya maisha yao na vizazi vijavyo.
Alisema utaratibu unaotumiwa katika kupata gesi hizo ni baada ya kuwathibitishia wasimamizi wa mradi huo kuwa na jiko la gesi katika kituo chao cha Mombasa karibu na Ofisi za Mufti Mkuu wa Zanzibar.
Hata hivyo alisema anashangazwa kuona tangu kuanza kwa mradi huo kumekuwa na idadi ndogo ya wananchi waliojitokeza kutaka kutumia nishati hiyo jambo ambalo ni tofauti na nchi nyengine.
Alisema inawezekana tatizo la wananchi wa Zanzibar kuwa na ghofu ya kutumia nishati hiyo kutokana na kutofahamu elimu ya matumizi ya majiko ya gesi lakini mradi wa HIMA umekuwa ukitoa elimu kabla ya mhusika kukabidhiwa vifaa vyake.
Dk. Aseeid alisema kuwa mradi huo wa HIMA ni wa kwanza duniani kutokana na kutokuwepo duniani kote na waliamua kufanya hivyo ikiwa ni hatua itayowawezesha wananchi wa Zanzibar kutumia fursa hiyo.
Kwa upande wake waziri wa Kilimo na Mali Asili, Mansoour Yussuf Himid, alisema serikali itafikiria namna ya kuondoa ushuru kwa majiko ya gesi.
Waziri Mansoour, alisema kama serikali imekuwa ikitoa ushuru kwa wafanyabishara vya vifaa vya umeme zikiwemo taa maalum zenye gharama ndogo ni vyema ikaliangalia na hilo ili wananchi waweze kuifikia nishati ya majiko ya gesi.
Alisema ni kweli inawezekana kampeni ya kuwataka wananchi kutumia majiko ya gesi isifanikiwe kutokana na hivi sasa majiko hayo kuuzwa kwa gharama kubwa jambo ambalo humganya mwananchi kushindwa kununua majiko hayo.
Katika hatua nyengine Mkurugenzi wa Misitu na raslimali zisizohamishika Shehe Idrisa Hamdani, alisema Idara yake inajiandaa kukabiliana na vitendo vya uchafuzi wa mazingira kwa wachimbaji wa mchanga na wakataji wa miti kwa kutumia misumeno ya umeme.
Alisema tangu kuanza kwa zoezi hilo tayari gari sita za mchanga zimekamatwa ambazo zimetozwa faini ya shilingi milioni mbili misumeno 14 na magari ya punda 25 ambao walitozwa faini ya shilingi 300,000.
Thursday, 14 April 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment