Omar Yusuf: CCM haiyumbishwi na hila za mafisadi
Na Ismail Mwinyi
MJUMBE wa Kamati Kuu CCM, Omar Yussuf Mzee amesema chama hicho kikongwe nchini, hakitayumbishwa na wala kubabaishwa na hila za mafisadi.
Waziri huyo alitoa kauli hiyo wakati wa sherehe za uzinduzi wa mradi wa maji safi na salama katika Jimbo la Kikwajuni, sherehe zilizokwenda sambamba na kumpongeza Mbunge wa Jimbo hilo Hamad Yussuf Masauni.
Alisema mafisadi hawana nguvu za kukitambia chama hicho na wasidhani kuwa wanaweza kukidhoofisha kwani CCM iko imara, haitishiki na wala kushughulishwa na mafisadi.
Mzee aliwaeleza wanachama wa Jimbo hilo kuwa Chama cha Mapinduzi, si Chama cha wababaishaji bali ni chama kuendeleza misingi yake ya kuwajali wakulima, wafanyakazi na wanyonge.
Alisema uamuzi wa chama hicho kujivua gamba kwa kujiuzulu sekritarieti ni uamuzi mzuri na wa busara ambao unalenga kuleta maendeleo na mabadiliko ndani ya chama hicho.
Aidha waziri huyo alitoa wito kwa viongozi mafisadi kwenye ngazi za matawi, wadi na majimbo nao kujivua gamba kwa kujiondosha kwenye nyazifa kabla ya kutimuliwa.
Alisema endapo watajiondosha wenyewe watakisaidia chama hicho na wanachama kurejesha imani na kukitumikia chama chao.
Sambamba na hilo aliwataka wanachama na wapenzi wa chama hicho kutokubali kuongozwa na viongozi mafisadi wasio na uchungu na chama ili kuepusha kutokea kwa mgawanyiko wa wanachama wake.
Mzee aliwataka wanachama wa CCM wa jimbo hilo kuongeza mashirikiano na viongozi wao na kuachana na maneno ya mafisadi wasiopenda maendeleo ya jimbo hilo.
Aidha waziri huyo aliwapongeza viongozi na wanachama wa Jimbo hilo kwa kuanzisha mradi wa maji safi na salama ambapo alisema hatua hiyo ni hatua mojawapo ya utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Waziri Mzee alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza kuimarisha mradi huo ili kuweza kutoa huduma hiyo kwa wananchi wote wa mjini na vijijini.
Nae Mbunge wa Jimbo hilo Hamad Yussuf Masauni, alimueleza waziri huyo kuwa licha ya kuweza kutatua tatizo hilo la maji jimboni hapo mradi huo utaendelea na shughuli zake za kuchimba visima vya ziada pamoja na kuvisaidia vikundi vya ujasiriamali vilivyopo jimboni hapo kwa lengo la kujikomboa na hali ngumu ya umasikini.
Thursday, 28 April 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment