Wanafunzi wasio walemavu kufundishwa lugha ya alama
Na Halima Abdalla
WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa kushirikiana na Jumuia ya Watu wenye ulemavu wa akili Zanzibar (ZPDD), imeandaa mafunzo juu ya ufahamu wa lugha za alama kwa wanafunzi ili yaweze kuwa na mawasiliano ya karibu kati ya wanafunzi waliokuwa viziwi na wasio viziwi wanapokuwa darasani.
Akizungumza na waandishi wa habari skuli ya Mwanakwerekwe ‘F’, Msimamizi wa mafunzo ya lugha za alama Ameir Khatib Hassan, alisema mafunzo haya yanasaidia sana kupata uelewa na ufahamu kwa wanafunzi waliokuwa viziwi na wasiokuwa viziwi kuweza kuwasiliana pamoja na mwalimu anapofundisha kuweza kuelewana.
Aidha alisema wanafunzi wanapopatiwa elimu ya lugha za alama inasaidia kuhamasika kutokana na ule mchanganyiko kwa wanafunzi wanapokuwa madarasani na kuzungumza kwa lugha za alama na kujenga ukaribu na urafiki kati yao.
Nae mwalimu wa lugha za alama katika Skuli ya Mwanakwerekwe ‘F’, Kazija Khatib Juma, alisema wanapofundisha lugha za alama wakiwa madarasani wanakabiliwa na ukosefu wa vifaa vya ufundishaji kwa wanafunzi viziwi ikiwemo kioo cha kuweza kuona matamshi yanavyotoka na kuweza kumsaidia mwanafunzi kufahamu.
Aidha alisema wanakabiliwa na uhaba wa vifaa vya kukalia baadhi ya madarasa wanafunzi wanalazimika kukaa chini kutokana na kukosekana kwa madawati.
Kwa upande wake Msaidizi Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Mwanakwerekwe ‘F’, Asha Mtaji Hassan, alisema idadi ya wanafunzi wenye mahitaji maalum katika skuli yake kila mwaka inaongezeka ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo wazazi walikuwa hawako tayari kuwatoa watoto wao kwa ajili ya kupata elimu.
Alisema kwa sasa wazazi na walimu wamekuwa na ushirikiano mzuri na wa karibu na wazee wamekuwa wakifuatilia vizuri maendeleo ya watoto wao.
Alisema mpaka sasa katika skuli yake robo tatu ya walimu wote wameshapatiwa mafunzo ya lugha za alama na pia wamekuwa na kipindi maalum kwa ajili ya kufundishana kwa walimu wote.
Aidha alitoa wito kwa Wizara ya Elimu kujali hali ya watoto wenye mahitaji maalum pamoja na kuthamini kitengo cha elimu mjumuisho.
Katika mafunzo hayo jumla ya wanafunzi 101 walipatiwa mafunzo hayo ya lugha za alama ikiwemo watatu kutoka Skuli ya Darajani, watatu kutoka Dimani na 95 kutoka skuli ya mwanakwerekwe ‘F’.
Mafunzo hayo ya siku tano yameandaliwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa kushirikiana na Jumuia ya watu wenye ulemavu wa akili Zanzibar (ZPDD), chini ya ufadhili wa shirika la (NFU) kutoka Norway.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment