Uwekezaji isiwe kisingizio kuharibu Mji mkongwe
Na Mwanajuma AbdiSERIKALI imeshauriwa kutokubali kushawishiwa wa wawekezaji wanaotaka kuwekeza miradi itayohatarisha urithi wa kimataifa wa Mji Mkongwe, ambao unachangia asilimia kubwa ya pato la taifa.
Ushauri huo umetolewa jana, Mtaalamu aliyeandaa kitabu cha Mpango Mkuu wa Uhifadhi, Prof. Saad Yahya katika sherehe za siku ya urithi wa kimataifa ulimwenguni, ambayo huadhimishwa kila ifikapo Aprili 18 duniani kote.
Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wananchi, Kiuchumi na Ushirika, Haroun Ali Suleiman alikuwa mgeni rasmi ambapo alizindua kitabu hicho kilichoandaliwa na Prof. Saad kutokana na mawazo na michango ya wakaazi wa mji huo.
Prof. Saad alisema wawekezaji wanaokuja kuwekeza nchi sio kama wafukuzwe lakini pia waangaliwe kwa makini miradi wanataka kuwekeza hasa katika mji huo ili wasije kuharibu haiba na hadhi yake na kuondolewa katika orodha ya urithi wa kimataifa.
Alifahamisha katika Mji Mkongwe maeneo mengi ya wazi yameuzwa kwa wawekezaji hali ambayo inachangia watoto kukosa sehemu za michezo na maeneo ya kujipumzisha.
Prof. Saad alieleza urithi wa Mji Mkongwe sio nyumba bali unabeba mambo mbali mbali ikiwemo mila, utamaduni, muziki na mavazi, ambapo katika maoni ya wananchi waliyoyatoa wamelalamikia suala zima la mavazi yanayovaliwa kuwa hayaendani na silka na tamaduni za Wazanzibari.
Naye mgeni rasmi Waziri Haroun, alihimiza utunzaji wa mji huo kwani una historia kubwa, ambapo baadhi ya nchi kama Qatar na Oman wana miji imefanana na Mji Mkongwe wa Zanzibar katika ujenzi wa nyumba zao huku zikiwa zimewekwa boriti na kujengwa kwa udongo na chokaa.
Alieleza haiwezekani kuwaacha watu wachache kuharibu mji huo wenye hadhi kubwa, huku akiishukuru Sweden kufadhili mji huo, ambapo aliwataja wafadhili hao wamekuwa wakisaidia msaada mkubwa katika miradi mbali mbali ya Serikali kupitia nishati na elimu imewezesha kufikia asilimia 100 ya mafanikio ya kunyanyua kiwango cha elimu nchini.
Nae Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, Ali Juma Shamuhuna alivipongeza vyombo vya habari na kuvitaka viendelee kutangaza mji huo kutokana na kuwa na vivutio vingi vya kitalii.
Nae Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezaji wa Mji Mkongwe, Issa Sarboko Makarani alisema siku hiyo katika nchi zenye urithi huambatana na kuwashirikisha wanafunzi katika sanaa ya uchoraji, matengenezo ya nyumba zilizochakaa na maandamano hufanyika kwa kuwashirikisha wananchi.
Alisema Prof. Saad ni mzaliwa Malindi Zanzibar lakini alipata elimu ya juu nje ya nchi, ni mdau na mkereketwa wa mji mkongwe hadi kuweza kuandaa kitabu hicho kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mji Mkongwe na Wataalamu kutoka Tanzania Bara na wataalamu wa Kenya.
Akifunga mkutano huo Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, Mwalim Ali Mwalim alitahadharisha kuenziwa na kuhifadhiwa mji Mkongwe wa Zanzibar ili ubakie katika orodha ya UNESCO kwani nchi kama Ujerumani imeondolewa baada ya kupoteza sifa hali inayosababisha kupoteza mamilioni ya fedha zinazotokana na mapato wa mji wake kwa kutembelewa na watalii.
No comments:
Post a Comment