Tuesday, 26 April 2011

WALIMU WAPEWE STADI KUWAEPUSHA MIMBA WANAFUNZI

Walimu wapewe stadi kuwaepushia mimba wanafunzi

Na Mwandishi Wetu, Dar
CHAMA cha Walimu Wanawake (TAWOTEA), kimependekeza serikali ilipe kipaumbele suala la elimu ya maadili na stadi za maisha katika vyuo vya ualimu ili kuepusha walimu kuwapa mimba wanafunzi.
Mkurugenzi mtendaji wa TAWOTEA, Neema Kabale alisema utovu wa maadili kwa walimu unasababishwa na udhaifu uliopo katika vyuo vya ualimu ambapo suala la kuwajengea waalimu misingi ya maadili ya kazi yao halipewi uzito unaostahili.
Alisema walimu wana kazi nyeti ya kujenga maadili mema kwa wanafunzi, serikali inapaswa kuhakikisha vyuo vya ualimu vinakuwa na wawezeshaji makini wa kuwajengea walimu maadili mema yanayotakiwa katika kazi yao ili wawe mfano kwa jamii.
Alifahamisha kuwa mwalimu anayekuwa chuoni miaka miwili au zaidi, kama chuo chake kimejiandaa vyema kumjenga kimaadili atakuwa amewiva na atakapokuwa kazini, kama ufuatiliaji wa maadili unafanyika kikamilifu, hatothubutu kujihusisha na mambo yaliyo kinyume na maadili ya kazi yake.
Akizungumza katika mahojiano maalum na TAMWA kuhusu chanzo cha walimu kuwapa mimba wanafunzi, Mkurugenzi huyo wa TAWOTEA alisema walimu wengi siku hizi wamepotoka kimaadili kwa sababu vyuo vingi vinavyofundisha kazi ya ualimu vinafanya kazi hiyo kwa mtindo wa “bora liende”.
Alitaja jambo jengine linalofanya walimu kukosa maadili na hivyo baadhi kujiingiza katika mapenzi na wanafunzi kuwa ni walimu kutopatiwa mafunzo mara kwa mara kuhusu stadi za maisha ili kuweza kujiepusha na vishawishi vinavyotokana na mazingira yanayobadilika.
Kabale alisema mwalimu anaweza kufanya kazi hata kwa kipindi cha miaka 20 bila kupatiwa mafunzo au stadi zozote zenye kumsaidia kujikumbusha masuala ya maadili ya kazi yake.
Mkurugenzi alisema kuwajengea uwezo waalimu walioko kazini kuhusu stadi za maisha zinazoweza kuwasaidia kuepuka vishawishi vya kufanya mapenzi na wanafunzi kunaweza kufanywa na taasisi, mashirika yasiyo ya kiserikali, vyama vya walimu na vyombo vya habari.
Alifahamisha kuwa suala la kupambana na tatizo la mimba maskulini linahitaji serikali kuweka rasilimali zaidi kuboresha vyuo vya ualimu na wadau wengine nje ya vyuo kuwa wabunifu na kujitolea kufanya shughuli zitakazoelimisha na kuhamasisha wale wote wanaofanya mapenzi na wanafunzi kuacha tabia hiyo.
Utafiti wa habari zinazochapishwa na magazeti kuhusu masuala ya mimba mashuleni unaonesha kuwa katika kipindi cha miezi minne kuanzia Disemba 2010 hadi mwisho wa mwezi Machi mwaka huu matukio 11 ya wanafunzi kupata ujauzito yalihusisha walimu.
Aidha tatizo la wasichana kukatisha masomo kutokana na mimba ni kubwa hapa nchini, ambapo kwa mujibu wa taarifa za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, katika kipindi cha miaka mitano, 2004-2008, jumla ya wanafunzi 28,590 wakiwepo 11,599 wa sekondari na 16,991 wa skuli za msingi, walikatisha masomo kwa kupata mimba.

No comments:

Post a Comment