Saturday 30 April 2011

CHADEMA YAISHITAKI BAJETI KWA WANANCHI.

CHADEMA yaishitaki bajeti kwa wananchi

Na Jumbe Ismailly,Singida
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilayani Singida kimeanza ziara ya kuwaelezea wananchi wa jimbo la Singida Magharibi namna madiwani, walivyopitisha mapendekezo ya bajeti ya mapato na matumizi ya zaidi ya shilingi bilioni 29,na kushindwa kuhoji zaidi ya shilingi milioni mia sita zilivyotumika.
Mbunge wa viti maalumu (CHADEMA) Christowaja Mtinda alitoa kauli hiyo alipokuwa akiongea kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Puma,wilayani Singida.
Mbunge huyo alisema madiwani wa CCM kwa kutumia uwingi wao waliungana na bila kujali matatizo ya wananchi kwa kupitisha zaidi ya shilingi bilioni 29 kwa mwaka 2011/2012.
Kutokana na hatua hiyo Chadema wanatarajia kumfikisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo kwa wananchi ili akawaeleze alipozipeleka asilimia ishirini ya fedha za fidia ambazo ni zaidi ya shilingi milioni mia sita zilizotolewa na serikali kuu kwa ajili ya kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo.
Mtinda ambaye ni Waziri kivuli wa wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi alifafanua kuwa Mei mosi mwaka 2002 serikali ilifuta ushuru wa mazao, licha ya kwamba bado kuna vizuizi vingi kwenye vijiji vya wilaya hiyo.
Kwa mujibu wa mbunge huyo ushuru huo wa mazao uliofutwa ulikuwa chanzo kikubwa cha mapato katika vijiji na kuongeza kwamba serikali kwa kulitambua hilo ikalazimika kurejesha asilimia ishirini ya mapato hayo kama fidia kwa kila mwaka.
Aliweka wazi mbunge huyo kwamba katika mwaka wa fedha wa 2008/2009 ilipokea kutoka serikali kuu zaidi ya shilingi milioni 247 zilizotakiwa kwenda vijijini kama fidia kwa ajili ya kufanikisha shughuli za maendeleo.
Hata hivyo Mtinda hakusita kuwafahamisha wananchi wa kijiji cha Puma kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2010/2011 wilaya hiyo ilipokea zaidi ya shilingi milioni 283 kama fidia za vyanzo mbalimbali vya mapato vilivyofutwa hazikupelekwa katika vijiji kama zilivyokusudiwa.
Alisema kwa mwaka huu Halmashauri hiyo imeomba zaidi ya shilingi milioni 163 kama fidia za vyanzo mbalimbali vya mapato kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012.

No comments:

Post a Comment