Friday, 8 April 2011

KIKWETE AIMONGONYOA CHADEMA MBEYA.

Kikwete aimong’onyoa CHADEMA Mbeya

Mwenyekiti, katibu mwenezi wapewa kadi Dodoma
Na Rajab Mkasaba, Dodoma

MWENYEKITI wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete, jana aliwakabidhi kadi za CCM wanachama wapya 150 kutoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Mbeya waliowakilishwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho Samuwel Chitambula na Katibu Mwenezi wa Wilaya ya Ileje, Henry Kayuni.

Mkutano maalum wa kuwakaribisha Wajumbe wa Kamati Kuu na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, uliwatambulisha wawakilishi hao na kukabidhiwa kadi za CCM mbele ya viwanja vya Makao Makuu ya Chama hicho Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.

Akiwakaribisha katika Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete aliupogeza Mkoa wa Mbeya na wanachama hao kwa uwamuzi wao sahihi wa kujunga na CCM kutokana na kuwa ni chama kinachoaminika na kinachokwenda na wakati.

Mapema, Mjumbe wa NEC Taifa kutoka Mkoa huo wa Mbeya Profesa Mark Mwandosya alieleza kuwa kujiunga kwa wanachama hao wapya kutoka Chama cha CHADEMA, kunadhihirisha CCM ilivyo imara.

Naye Samuel Chitambula aliyejiunga na CCM na aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA, Mkoa wa Mbeya ambaye pia, anatokea katika ukoo wa Chifu Mkuu wa Mkoa huo, alieleza kuwa ameingia CCM kwa ridhaa yake akiwa na akili timamu.

Alisema kuwa chama anachotokea hakuweza kupata mwelekeo ambao unapaswa kuweza kuwaheshimu wazee na wakubwa waliokuzidi pamoja na kukosa mshikamano na badala yake kushuhudia dharau.

Chitambula alieleza kushangazwa na chama alichokihama kuwa hawamuheshimu Rais Jakaya Mrisho Kikwete ambaye ni rais halali aliyechaguliwa kwa kura nyingi na wananchi.

Alisema hivi sasa yuko tayari kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi Mkoa huo wa Mbeya kwa vile yeye ndio muanzilishi “Ukitaka kubomoa nyumba basi ni vizuri umtafute fundi aliyejenga”,alisistiza Chitambula.

Naye aliyekuwa Katibu Mwenyezi wa Wilaya ya Ileje, ambaye aliyejiunga na CCM, Henry Kayuni alieleza kuwa kikubwa aichokipata katika chama alichotoka ni kukabiliwa na mzigo wa madeni kwa kutumia kiasi kikubwa cha fedha kwa lengo lake la kugombania nafasi ya Ubunge ambayo aliikosa.

“Nimerudi kama mtoto mpotevu aliyerudi kwa baba yake na mnisamehe kwa yote niliyofanya, Rais Kikwete anafaa kwa asilimia mia moja na viongozi wote mliochaguliwa wakiwemo Wabunge wa CCM mnafa kwa asilimia mia moja akiwemo Mbunge wangu wa Ileje kwani kanisaidia hadi nauli ya kujia huku”alisema Kayuni.

Aidha, Kayuni aliomba mchango kwa viongozi wa CCM ili aweze kulipa deni hilo ambalo kesi yake iko mahakamani na kusisitiza kuwa atafanya kazi pamoja na wanaCCM hadi mwisho wa maisha yake.

Viongozi wa CCM Taifa wako Mkoani Dodoma kwa lengo la kuhudhuria vikao mbali mbali vya chama hicho.

No comments:

Post a Comment