Sunday 24 April 2011

MAMA SHEIN; WANACCM CHAGUENI VIONGOZI WAKWELI WAADILIFU.

Mama Shein: WanaCCM chagueni viongozi wakweli, waadilifu

Na Mwanajuma Abdi
MKE wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mama Mwanamwema Shein amewataka wanaCCM kuchagua viongozi waadilifu na wakweli katika uchaguzi wa chama hicho mwakani kwa ajili ya kujiandaa na ushindi wa uchaguzi mkuu wa 2015.
Mama Shein aliyasema hayo jana, katika viwanja vya skuli ya Kiongoni Makunduchi kwenye mkutano maalum wa wanavikundi vya ushirika vya SACCOS katika shehia mbali mbali, ambapo ikiwa ni sambamba na ziara ya siku moja ya kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Makunduchi kwa kukipatia ushindi chama hicho katika uchaguzi wa mwaka jana.
Mapema alitembelea na kuweka jiwe la msingi ya Mwelekeo Mwema SACCOS ya Mtende, ambapo alichangia shilingi 300,000 na kufungua ofisi ya Mkombozi SACCOS ya Kizimkazi Dimbani pia alikabidhi shilingi 200,000 kwa ajili ya kuendeleza mtaji wa ushirika huo pamoja na kukutana na vikundi ya ushirika vya shehia ya mbali mbali huko Kiongoni Makunduchi.
Alisema wanaCCM wajiandae na uchaguzi wa ndani ya Chama hicho utaofanyika mwakani ili kuweza kuchagua viongozi wataoweza kuendeleza ushindi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, pamoja na kuwahimiza wazazi kuwashajiisha vijana waliofikia umri wa kwenda kujiandikisha katika daftari la wapiga kura waende.



Alieleza uchaguzi umemalizika kwa utulivu na amani, ambao umeendeshwa kwa uhuru na haki na kufanikisha kushika madaraka Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, hali ambayo umesaidia ulimwengu mzima kuipongeza nchi kwa mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika kudumisha amani nchini, hivyo alisisitiza umoja na mshikamano uendele kuwepo kwa ajili ya maendeleo endelevu.
Akizungumzia kuhusu SACCOS, alisema Serikali inatambua mchango mkubwa wa kinamama na akinababa kupitia vikundi vya ushirika na ndio maana ikawekwa Wizara maalum ya kushughulikia masuala hayo kwa ajili ya kukuza uchumi na kupunguza umasikini.
Alisema wananchi wamejikita katika masuala ya kuwanyanyua kiuchumi katika sekta mbali mbali zikiwemo za kilimo, biashara na ufugaji, ambapo hiyo ni hatua kubwa katika kuwakomboa na umasikini.
Aliwapongeza wanaSACCOS hao kwa juhudi zao kubwa za kuanzisha ushirika huo katika kujikomboa kiuchumi na kimaisha, ambapo aliwahimiza wadumishe umoja na mashirikiano kwani bila hayo hawatoweza kufikia malengo waliyojipangia.
Mama Mwanamwema Shein aliwahimiza wanaSACCOS kuwa wawazi katika masuala ya fedha ili ushirika huo uweze kupiga hatua, sambamba na kuwashajiisha wanaokopa warudishe pesa kwa wakati ili na wenzao wakopeshwe.
Nae Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mama Asha Seif Iddi, aliahidi kuwasaidia matreki suti kwa kikundi cha mazoezi cha Kizimkazi Dimbani, pamoja na kutoa wito kwa vikundi vya Ushirika kuungana pamoja ili wawe wengi na waweze kukopesheka katika mabenki.
Waziri wa Kazi, Uwezeshaji wananchi, Kiuchumi na Ushirika ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Makunduchi, Haroun Ali Suleiman alitilia mkazo umuhimu wa kuunganisha vikundi vya ushirika ili vifikie vitatu vikubwa katika Jimbo hilo kwa lengo la kupata misaada mingi na kuweza kukopesheka katika mabenki.
Alisema katika jimbo hilo wanaCCM hawana masihara, ambapo wanapotoa ahadi lazima watimize kwa kuwapa kura zote wagombea wa Chama cha Mapinduzi kama walivyofanya uchaguzi uliopita na ujao utakuwa hivyo hivyo.
Mapema wakisoma risala zao wanaSACCOS wa Kijiji cha Mtende, Makunduchi na Kizimkazi Dimbani walimshukuru Mama Mwanamwema Shein kwa kutimiza ahadi yake ya kwenda kuwashukuru baada ya kumaliza uchaguzi mkuu mwaka jana.
Hata hivyo baadhi ya wanaSACCOS walitaka kusaidiwa kupatiwa mafunzo, nyenzo za kumaliza jengo lao pamoja na kuongezewa mitaji, ambapo pia waliwapongeza Rais wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Mrisho na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein kwa kutimia miaka 47 ya Muungano wa Tanzania.
Nao kikundi cha michezo, waliwashajiisha wananchi kufanya mazoezi kwa ajili ya kujiweka vizuri kiafya na kuondokana kuonana na daktari mara kwa mara wakisumbuliwa maradhi mbali mbali.

No comments:

Post a Comment