Saturday, 16 April 2011

MAOFISA WATAKIWA KUANDAA TAARIFA SAHIHI

Maofisa watakiwa kuandaa taarifa sahihi

Na Zuwena Shaaban, Pemba

MAOFISA Mipango wa Idara na Taasisi zilizochini ya Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Pemba, wametakiwa kubadilika katika uandaaji wa taarifa na kufuata maadili ya kazi zao.
Ofisa Mdhamini Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Jokha Khamis Makame alieleza hayo alipokuwa akizungumza na maofisa hao katika ukumbi wa kiwanda cha Makonyo Wawi.
Alisema wakati umefika kwa kila mmoja kubadilika na taarifa zinazoandaliwa na maofisa hao ziwe sahihi na za uhakika ili malengo yaliyopo yaweze kufikiwa.
Ofisa huyo aliwataka maofisa hao kukaa pamoja na kubadilisha mawazo kwani kwa kufanya hivyo kutaweza kuzibadilisha taarifa hizo zinazoandaliwa na maofisa hao.
Alisema upo umhimu wa kuaandaa taarifa sahihi kwani ni nyenzo muhimu katika kupima ufanisi, uwajibikaji na usahihi wa utekelezaji wa majukumu.
Alieleza kwamba lengo la kukutana na watendaji hao ni kuwataka kufanya kazi zao kwa makini huku wakifahamu kuwa ofisi yao kuwa ni kioo kwa jamii kwa hiyo watendaji hao wawe na ufanisi mzuri katika kazi.
Alifafanua kuwa watendaji hao wakiwa pamoja wataweza kufanyakazi kwa uadilifu na umahiri mkubwa na kuwataka waungane pamoja katika kuleta ufanisi mkubwa katika kazi zao za kila siku.
Ofisa huyo aliwataka Maafisa hao kuweka mbele masuala ya kuweza kujifunza kwa kujipatia elimu kwani elimu ni muhimu wakati wote kwani elimu humsaidia mtu katika kutafakari na kutoa maamuzi sahihi ya kuweza kumsaidia kila dakika na kuweza kuchanganua mambo mbali mbali ya umuhimu kabisa.

No comments:

Post a Comment