Friday, 29 April 2011

MASHIRIKA YAWAANDAMA WALIMU 'VITANGI'

Mashirika yawaandama walimu ‘vitangi’

Na Mwandishi Wetu, Dar
VIONGOZI wa mashiriki sita yanayotetea haki za binadamu na maendeleo wamependekeza hatua zichukuliwe kurejesha maadili ya kitaifa na kuwaadhibu vikali walimu wanaowapa mimba wanafunzi.
Wamesema bila kuchukua hatua madhubuti kurejesha maadili ya taifa, sekta ya elimu itaendelea kushuhudia ongezeko la mimba maskulini na hivyo kukwamisha jitihada za taifa kuhakikisha watoto wote wanapata elimu ambayo ni haki yao ya msingi.
Wamesisitiza kuwa walimu wanaobainika kufanya mapenzi na kuwapa mimba wanafunzi wafukuzwe kazi, washitakiwe kwa kosa la kubaka na walazimishwe kulipa fidia za matunzo ya mtoto anayezaliwa.
Wamewahimiza wanafunzi hasa wasichana kuwafichua bila kuona woga au unyanyapaa walimu wote wanaofanya mapenzi na wanafunzi ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Kwa mujibu wa taarifa za wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, katika kipindi cha miaka mitano, 2004-2008, jumla ya wanafunzi 28, 590 wakiwepo 11,599 wa sekondari na 16,991 wa skuli za msingi, walikatisha masomo kwa kupata mimba.
Viongozi hao waliozungumza na TAMWA kwa nyakati tofauti wiki hii ni Mkurugenzi Mtendaji wa ForDIA, Bubelwa Kaiza, wa Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Ussu Mallya na wa Chama cha Wanawake Wanasheria (TAWLA) Ann Marie Mavenjina.
Wengine ni wa Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake (WLAC) Scholastica Jullu, wa shirika la Kutetea Haki za wanawake Kivulini lenye makao yake Mwanza, Maimuna Kanyamala na Mkurugenzi wa Utetezi na uboreshaji wa sera na shirika, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).
Utafiti wa habari zinazochapishwa unaonesha kuwa katika kipindi cha miezi minne kuanzia Desemba 2010 hadi mwisho wa mwezi Machi mwaka huu matukio 11 ya wanafunzi kupata ujauzito walimu ndio waliohusika.
Viongozi hao wanaharakati wamesema wanafunzi kukatishwa masomo kwa mimba kunasababisha madhara mengi kwa taifa ikiwa ni pamoja na ongezeko la ujinga na umaskini miongoni mwa wanawake, vifo vinavyotokana na ujauzito na maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI (VVU).
Utatifi wa kitaifa (Demographic Health Survey) uliofanyika mwaka 2010 unaonyesha vifo vya uzazi bado ni tatizo kubwa la kitaifa ambapo zaidi ya wanawake 8,000 wanakufa kila mwaka hapa nchini kutokana na sababu zinazoweza kuzuilika.
Kwa upande wa maambukizi ya VVU utafiti wa kitaifa uliofanyika 2007/2008 unaonyesha kuwa idadi ya asilimia 5.7 ya Watanzania wote wameambukizwa lakini wanawake na wasichana ndio wameambukizwa zaidi ambapo asilimia 6.6 ya idadi yao nchini wameambukizwa ikilinganishwa na asilimia 4.6 ya wanaume.

No comments:

Post a Comment