Saturday, 30 April 2011

MZEE MOYO AIBUKA TENA

Mzee Moyo aibuka tena

Ashangaa kusikia Muungano hauna hati
Asema alimuona nazo mzee Karuma
Na Mwantanga Ame
WAZIRI wa Kwanza wa elimu katika serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hassan Nassor Moyo, amekuja juu na kueleza kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar una hati.
Mzee huyo mwenye kuheshimika, alieleza hayo kwenye mahijiano maalum na kituo cha redio cha sauti ya Ujerumani.
Alisema madai yanaibuka hivi kuwa hati ya Muungano haipo hayana ukweli na wanaosema haipo hawafahamu ukweli juu ya suala hilo, na kubainisha kuwa anaamini hati hiyo ipo.
Mzee Moyo alisema anashangazwa sana na hoja zinazoletolewa hivi sasa kudaiwa hati ya muungano haipo wakati yeye alikuwa shahidi aliyemshuhudia Mzee Karume akiweka saini kwenye hati hiyo.
Ushuhuda mwengine aliyoutoa mzee Moyo kuelezea uwepo wa hati hiyo ni hatua ya mzee Karume kuwafikishia hati hiyo mbele ya Baraza la Mapinduzi baada ya kuweka saini huko Tanganyika.
“Mkataba wa Muungano niliuona ukiwa umetiwa saini, kwani hati hizo baada ya kutiwa saini ilikabidhiwa serikali ya Zanzibar” alisema Mzee Moyo.
Aidha alipinga vikali kwa kusema wakati baraza hilo likipokea hati hizo za Muungano, hakuwepo aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Wolfgang Dorado siku ya kikao hicho.
Akizungumzia hoja zilizojitokeza wakati wa mjadala wa rasimu ya Katiba mpya, alisema rasimu hiyo ilipaswa kuondolewa kutokana na kujitokeza kasoro nyingi ambazo hazikuwa zinatoa haki kwa maslahi ya Zanzibar.
Hata hivyo alisisitiza suala la msingi ni kuwepo mjadala wa katiba mpya ya Muungano ambapo ndio moja ya suluhu ya mambo yote ambapo wananchi watatumia haki hiyo kuweza kuchagua yepi wanayoona yanafaa kwenye Muungano uliopo.
Alisema katika mambo ya Muungano hivi sasa kuna mambo mengi yanahitaji kuangaliwa kwani makubaliano ya awali yaliletwa yakiwa na mambo 11 ambayo kupitishwa kwake yalifanyika zaidi kwa makubaliano ya viongozi waliopo wakati huo.
Alisema hivi sasa tayari kuna vijana wenye mawazo ya kustawisha Zanzibar katika muundo wa Muungano na ni lazima wapewe nafasi kuelezea matakwa yao ili baadae serikali iyazingatie kwa maslahi ya taifa kwa yale ambayo yataonekana kuwa na manufaa.
Kwa upande wake Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Zuberi Kabwe katika mjadala huo alisema pande zote za Muungano zimekuwa na lawama kwani wamebaini kuwapo kwa baadhi ya mambo yanalalamikiwa.
Alisema kilichotokea ni kuzuiliwa kwa hoja ya Muungano, akisema wananchiliwe waalizungumze na pia wasema aina ya Muungano unaowafaa.
Zitto alisema Zanzibar inataka mafuta na gesi kutolewa katika mambo ya Mungano jambo lenye kuwezekana kwani haiwezekani uchimbaji wa madini ya dhahabu mafuta na gesi kuwa ni mambo ya Muungano wakati hakuna faida inayokwenda Zanzibar.
Mjadala wa Muungano umekuwa ukikuwa siku hadi siku katika vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi ambapo mwanzoni mwa wiki hii Muungano ya Tanganyika na Zanzibar ulitimiza miaka 47 sherehe ambazo zilifanyika Mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na umati wa wananchi.

No comments:

Post a Comment