Tuesday, 26 April 2011

FIKRA ZA KUVUNJA MUUNGANO ZAPINGWA.

….Fikra za kuvunja Muungano zapingwa

• Lipumba: Ni dhambi kubwa
• Himid Ameir: Ni utashi wa wachache
• Fatma Karume: Wasioutaka wana lao jambo
Na Mwantanga Ame
WAKATI watanzania jana wakiadhimisha miaka 47 ya Muungano, Mwenyekiti wa Chama cha CUF, Profesa Ibrahim Lipimba, amesema wenye kutoa mawazo ya kutaka kuvunjwa kwa Muungano wasifikirie hata siku moja kuleta dhana hiyo kwani imejaa dhambi na haina faida kwa watanzania.
Profesa Lipumba aliyasema hayo jana wakati akitoa mawazo yake katika maadhimisho ya sherehe hizo zilizofanyika katika kiwanja cha Amaan Mjini Unguja ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Tudumishe Muungano matunda ya miaka 47 ya Mapinduzi na miaka 50 ya Uhuru’.
Lipumba alisema, Muungano uliopo ni mzuri, lakini haipaswi kutumia changamoto zilizojitokeza kwa kujenga hoja ya kuuvunja kwani hiyo ni dhana iliyojaa dhambi na haina faida kwa watanzania pindipo wakishikilia wazo hilo.
Alisema wazo la kutaka kuvunjika kwa Muungano ni baya kwani linaweza likaleta athari kubwa kwa baadhi ya watanzania kutokana na kuwa tayari wamezaliwa wakiwa ndani ya muungano bila ya kuzingatia maeneo waishio nchini Tanzania.
Akitoa mfano alisema hivi sasa kuna Wazanzibari 400,000 hawana haki ya kupiga kura Zanzibar, ambao wamezaliwa Tanzania bara na watu wa Zanzibar ambao hawapigi kura Bara kutokana na sheria zilizopo jambo ambalo ikiwa muungano utavunjika hawatakuwa na sehemu ya kushika.
“Kuna athari kubwa ya kibinadamu itayotokea kama tukianza kujenga hoja za kutaka kuvunja muungano na nnawaomba wananchi wasifikirie jambo hili hata siku moja kwani bado kuna jambo la kheri katika Muungano” alisema Lipumba.
Akiendelea alisema ingawa ni ukweli rasimu iliyotayarishwa kwa ajili ya kukusanya maoni ya mchakato wa kupatikana katiba mpya ilikuwa na kasoro zake lakini bado watanzania wanahitaji kutumia nafasi zao kutoa maoni ambayo yatakidhi mahitaji na sio jazba za kutaka kuvunjwa kwa muungano.
Alisema jambo linalotakiwa kufanywa ni kuangalia namna ya vipi wataweza kukabiliana na changamoto zilizopo na kufanyiwa mabadiliko ambayo yataweza kuufanya Muungano kuwa katika hali nzuri miaka 50 ijayo. .
“Jambo la kheri kuwa na muungano ni kweli kuna matatizo lakini yanaweza kutatuliwa na kurekebishwa na kukawepo utaratibu mzuri kupata katiba nzuri sio kuvunja Muungano, kama tunaweza kuliangalia kwa mfumo mwengine basi hayo ndio mambo ya kuyatazama sio usiwepo… hapana” alisema Lipumba.
Nae Mzee wa CCM Hamid Ameir Ali, akizungumzia juu ya mtazamo wake katika sherehe hizo alisema hoja za kutaka kuvunjwa kwa muungano ni utashi wa kilimwengu na haupaswi kufuatwa kwa wanaotoa ushawishi wa aina hiyo.
Alisema hilo linapaswa kuzingatiwa kutokana na Muungano uliopo ni wa kupigiwa mfano kwani ulitokana na nguvu ya kushindwa kwa wakoloni kuzitawala nchi mbili hizi na kuzifanya kuwa huru.
Alisema Changamoto zinazojitokeza za kujengewa dhana hizo ni ukuwaji wa maendeleo jambo ambalo watantazia watapaswa kuona kuwa yanayojitokeza ni maendeleo ya kuudumisha muungano ili waweze kupata manufaa zaidi na sio kuwaza kuuvunja.
Nae mjane wa Muasisi wa Muungano Zanzibar, Mama Fatma Karume, alisema Muungano wa Tanzania ni wa kupigiwa mfano kwani baadhi ya mataifa ndio kwanza wanafahamu umuhimu wa kuunganisha nchi zao.
Alisema kama baadhi ya mataifa yameweza kuunganisha nchi zao na kuwa na aina ya fedha zao kwanini Muungano wa Tanzania nao usionekane kuwa na faida na hoja za kutaka kuuvunja ni sawa na kurejesha nyuma maendeleo hayo.
Mama Fatma alisema hoja ambazo sasa zimekuwa zikitolewa kutaka kuvunjwa kwa muungano hazina msingi na wanaoleta mawazo hao ni kwamba inaonekana kuwa wana jambo lao.
Nae Waziri wa mambo ya Nje Ushirikiano wa Kimataifa Bernard Membe, alisema Muungano wa Tanzania ni urithi ulio bora kwa wananchi wa Tanzania hasa kwa kizazi cha sasa na haitapendeza kuona urithi huo unapotezwa.
Alisema changamoto ni kweli zipo na hazihitaji kupuuzwa kutokana na kukua kwa maendeleo na jambo ambalo linahitajika kufanywa kwa hivi sasa ni kupatiwa ufumbuzi ili uweze kwenda sambamba na matakwa ya wananchi.
Wananchi mbali mbali walishiriki katika sherehe hizo zilizoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete ambapo aliweza kukagua gwaride lililotayarishwa na vikosi vya Ulinzi na Usalama ambapo liliweza kuonesha umahiri kwa kutembea mwendo wa pole na haraka kiwanjani hapo na kufanya kushangiriwa kwa vikosi ambavyo vilionekana kufanya vizuri.
Vikosi hivyo ni vya JWTZ, Magereza, Polisi, Askari wa Majini, JKT, KMKM, Mafunzo, JKU na KVZ vilivyokuwa na gadi za askari wanaume na wanawake viliongozwa na kikosi cha bendera na bendi za vikosi hivyo.
Kwenye kiwanja hicho kilionekana kujaa wananchi waliokuwa wakishereheka kwa wakati huku wakipeperusha mabofu yaliokuwa na rangi ya Muungano na kuinua juu vitambara maalum vya bendera ya Muungano na kundi kubwa la wanafunzi wa skuli mbali mbali za Zanzibar waliovalia fulana maalum za muungano ambapo kwa muda wote walionekana kushajiisha sherehe hizo kwa kupiga makofi kwa mtindo maalum.
Viongozi wengine walioshiriki katiks sherehe hiyo ni pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bilal, Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.
Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowasa, nae pia alishiriki katika sherehe hizo na Rais wa Tanzania Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour Juma na Waziri Kiongozi Wastaafu Ramadhan Haji Faki na Shamsi Vuai Nahodha na wake wa viongozi hao Mwaziri wa SMZ na SMT na Makatibu Wakuu na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania na Zanzibar.

No comments:

Post a Comment