Mwera, Kianga uhalifu juu
Na Ramadhan Himid, POLISI.
KAMISHNA wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa amewataka wananchi wa Mwera Meli sita, Mtofaani na Kianga kuanzisha kamati za ulinzi, usalama na ustawi wa jamii ili kupunguza uhalifu kwani takwimu zinaonyesha kuwa uhalifu umepanda kwa kasi katika maeneo yao wanayoishi.
Aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na kamati za ulinzi, usalama na ustawi wa jamii katika shehia za Mwera Meli sita, Mtofaani na Kianga katika mfululizo wa ziara zake za kutembelea shehia mbali mbali ili kuweka mikakati imara ya kukabiliana na uhalifu nchini.
Alisema takwimu zinaonesha kwamba mwaka 2009/2010 matokeo makubwa ya uhalifu yamepungua lakini kuna maeneo bado uhalifu wa uvunjaji, dawa za kulevya, wizi wa mazao, mifugo na uhalifu mwengine umekuwa ukipanda mno siku hadi siku.
Alisema kwa upande wa makosa ya uvunjaji kipindi cha mwaka huu 2011 mwezi Januari pekee makosa yaliyoripotiwa maeneo ya Mjini ni matatu(3) wakati Mwera na Kianga ni makosa 14 na mwezi Februari makosa ya uvunjaji Mjini ni kosa moja tu wakati Mwera na Kianga ni 16.
“Nimekuwa nikijiuliza masuali mengi kichwani mwangu kwa nini Mjini ambako kuna idadi kubwa ya watu uhalifu unapungua lakini maeneo ya Mwera na Kianga uhalifu umekuwa ukipanda kwa kiwango kikubwa, nadhani inatokana na nyinyi wenyewe kuwa hamjajipanga kwani huko Mjini Kamati za ulinzi na usalama zinafanya kazi na ndio maana wahalifu hao wanakimbilia maeneo yenu”, alisema Kamishna.
Alisema Kamati za Ulinzi na Ustawi wa jamii ni muhimili muhimu wa kutatua kero za uhalifu kwani zipo Shehia ambazo zilikuwa na matatizo sugu ya kihalifu lakini baada ya kuanzishwa kwa Kamati hizo Uhalifu umepungua.
Alibainisha kwamba iwapo Kamati hizo zitafanya vikao mara kwa mara, kupeana taarifa na kuzipatia ufumbuzi taarifa hizo, vitendo vya kihalifu vinaweza kutoweka lakini kama wataendelea kuoneana muhali miongoni mwao watajikuta wakiishi katika hali ya wasi wasi.
Aidha aliwataka wananchi hao kuunga mkono falsafa ya Polisi Jamii kwani Majeshi yote duniani yenye sura ya upolisi yamefanikiwa kupunguza uhalifu kwa kuwashirikisha wananchi, na kumtaka kila mwananchi ashiriki kikamilifu kwa nafasi yake aliyo nayo katika kukabiliana na uhalifu ambao umekuwa ukirejesha nyuma harakati za kiuchumi.
Alisema Polisi Jamii ni sera kama zilivyo sera za vyama na taasisi nyengine hivyo sera hiyo ni sera ya majeshi yote duniani inayotilia mkazo ushirikishwaji wa jamii katika kutatua kero za uhalifu, kwani bila ya kuwepo mashirikiano ya dhati kati ya pande hizo mbili suala la usalama litabakia kuwa ndoto.
Alisema Polisi Jamii/Ulinzi Shirikishi ni ushirikishwaji wa wananchi katika suala zima la kukabiliana na kero mbali mbali zilizomo ndani ya jamii yao inayowazunguka ili wananchi hao waweze kufanya shughuli zao za maendeleo kwa hali ya amani na usalama.
Kwa upande wake Diwani wa Wadi ya Mwera, Shani Omar Mbena alikiri kuwa uhalifu katika maeneo ya Mwera umekuwa mkubwa na hivyo wananchi hawanabudi kuyaunga mkono yale yote yaliyotolewa na Kamishna kwa faida ya kujilinda wao wenyewe na mali zao.
Diwani huyo alimpongeza Kamishna Mussa na kusema kwamba amekuwa ni mfano kwani tokea kuzaliwa kwake hajawahi kumuona Kamishna wa Polisi akipita kwa wananchi kusikiliza kero zao.
Friday, 29 April 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment