Monday 18 April 2011

PINDA SERIKALI YAKUBALI KUONDOA MSWADA WA KATIBA.

Pinda: Serikali yakubali kuondolewa Mswada wa katiba

• Asema viraka bado si tatizo
Na Mwantanga Ame
SERIKALI ya Tanzania imesema imeridhia maamuzi ya Bunge ya kutaka kuiongeza muda kamati ya kukusanya maoni kwa ajili ya kuuandaa utaratibu utaotumika kuandaa katiba mpya na wananchi hawapaswi kubeza hatua hiyo.
Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Kayanza Peter Pinda aliyasema hayo jana wakati akitoa hotuba yake ya kuliakhirisha Bunge la Jamhuri ya Muungano lililomaliza kikao chake Mjini Dodoma.
Mswada wa kuandaa Tume ya kuandika katiba mpya ulipelekwa bungeni na serikali kwa hati ya dharura ikiwa ni hatua ya kuweza kuifanya kamati ya katiba, sheria na Utawala ya Bunge kukusanya maoni yatayowezesha namna ya muundo utaotumika katika kuunda tume ya kutayarisha katiba.
Kupelekwa kwa mswada, wabunge waliliomba kuacha kuujadili rasimu hiyo hadi pale itapofikishwa kwa wadau na wananchi kutoa maoni yao na ili uweze kueleka zaidi.
Akitoa hotuba yake Pinda alisema serikali imekubaliana na maamuzi ya Bunge hilo na itahakikisha kila pendekezo yatakayotolewa yatafanyiwa kazi ikiwemo la kuandaa rasimu hiyo kwa lugha ya kishwahili pamoja na kuuchapisha katika magazeti yote ya hapa nchini.
Alisema kimsingi serikali imekubali kuiongezea muda kamati hiyo kwani kinachoonekana wananchi wameielewa vyema dhamira ya serikali yao katika kufanya mabadiliko ya katiba hiyo na ndio maana wameamua kutoa michango yao.
Alisema jambo la msingi ambalo wananchi wakati wakisubiri mchakato huo kuanza ni vyema wakashiriki kutoa maoni yao kwa amani na sio kubeza maendeleo yaliofikiwa kiasi ambacho kitasababisha kuwapo kwa uvunjifu wa amani.
Kuhusu hoja ya katiba ya Tanzania imeshatiwa viraka vingi alisema bado Tanzania katiba yake haijafanya vibaya kutokana na kuwepo kwa mataifa kadhaa ambayo yameizidi Tanzania kwa kufanya mabadiliko ya Katiba.
Akitoa mfano alisema serikali ya Afrika Kusini imefanya mabadiliko ya katiba yake mara 16, Marekani mara 27, na India mara 94 ambapo Tanzania mara 14 ambapo alisema kilichokuwa kinajengwa katika hoja hiyo ni dhana potofu.
Alisema serikali ya Tanzania kwa kuheshimu wanachi wake imekuwa ikichukua hatua kila pale inapoona haja ya kufanyika mabadiliko ya Katiba kama ilivyofanya mwaka 1992 kwa kukubali kubaduili katiba yake kwa lengo la kufuata mfumo wa vyama vingi.
Alisema jambo la msingi ambalo wananchi wanapaswa kulitekeleza ni kuona bado wanaiheshimu katiba iliyopo hadi pale itapopatikana Katiba mpya ambayo inatarajiwa kutumika miaka 50 ijayo.
Alisema matarajio ya kuletwa tena kwa mswada huo katika Bunge serikali inakusudia kufanya hivyo kikao kijacho cha bunge ambapo kinatarajiwa kuanza Juni 7,mwaka huu ambapo mchakato kamili wa serikali kuweza kupatikana kwa Katiba mpya unatarajiwa ufikie kikomo Aprili 2014.
Hata hivyo katika hotuba yake hiyo aliwahimiza wananchi kuliangalia soko la asali kwa kuanzisha ufugaji wa nyuki, kutokana na kuwepo kwa tija kubwa, kujihadhari na mvua, kudumisha amani, Halmashauri kuwalipa stahili zao walimu, na kutahadharisha jamii kuchunguza afya kutokana na kuongezeka kwa maradhi ya kansa, kisukari, na kuahidi kuwa serikali itahakikisha inalifanyia kazi tatizo la mitambo ya umeme ambapo aliahidi 2012 litamalizika.

No comments:

Post a Comment