Tuesday, 26 April 2011

MAALIM SULE AOMBA USHIRIKIANO KUHIFADHISHA KUR-ANI WATOTO

Maalim Sule aomba ushirikiano kuhifadhisha kur-ani watoto

Na Aboud Mahmoud
WAZAZI wa watoto wa kiislamu wameshauriwa kushirikiana na Jumuiya ya kuhifadhisha kur-ani Zanzibar ili vijana hao waweze kukitumia kwa ufasaha kitabu hicho.
Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya kuhifadhisha kur-aan, Suleiman Omar Ahmed ‘Maalim Sule’ katika mashindano maalum ya kuhifadhi kur-ani katika ukumbi wa salama uliopo hoteli ya Bwawani.
Maalim Sule alisema kuwa jumuiya pekeyake haiwezi kufanya kazi bila ya kushirikiana na wazazi wa wanafunzi hao ili waweze kukihifadhi uzuri kitabu hicho.
Alieleza kwamba ni vyema kwa wazazi kutoa mashirikiano ya dhati kwa kuweza kuwapa vijana muongozi mzuri wa kukitunza na kuhifadhi kur-an.
“Napenda kutoa ushauri kwa wazazi wenzangu kuwa bega kwa bega na jumuiya yetu ili tuweze kuwapa muongozo mzuri wa kitabu cha Quraan,”alisema Maalim Sule.
Akisoma risala ya ufunguzi wa mashindano hayo Maalim Faki alisema kuwa Jumuiya hiyo tangu kuanzishwa kwake imeweza kupata mafanikio mbali mbali ikiwemo kuweza kuhifadhisha wanafunzi msahafu mzima wapatao 100,kupatikana kwa nafasi za ushiriki wa mashindano ya kimataifa.
Nyengine ni kuitangaza nchi kimataifa na kupatikana vijana wenye vipaji vya kuhifadhisha kur-an.
Risala hiyo ilieleza kuwa jumuiya hiyo inakabiliwa na changmoto kadhaa ikiwemo mashirikiano madogo baina ya wazee na walimu.
Katika mashindano hayo Jumla ya wanafunzi kutoka katika kanda mbali mbali za Unguja walishiriki katika mashindano hayo ya kuhifadhi kur-ani.
Juzuu zilizoshindaniwa ni Juzuu 30,20,10 na 5 ambapo pia wanafunzi hao waliweza kushiriki kwa njia ya tashjii tahkik.

No comments:

Post a Comment