Thursday, 28 April 2011

RC AWAOMBEA MISAADA WAATHIRIKA MAFURIKO MOROGORO.

RC awaombea misaada waathirika mafuriko Morogoro

Na Nalengo Daniel, Morogoro
MKUU wa Mkoa wa Morogoro Luteni Kanali Msataafu Issa Machibya, amewaomba wafanyabiashara, tatasisi zisizo za serikali, mashirika ya dini na watu binafsi kuwasaidia wananchi 6,643 walioathirika na mafuriko yaliyotokea wilayani Kilombero mkoni hapa.
Mkuu huyo alitoa ombi hilo jana mkoani hapa kwenye kikao cha pamoja kati ya uongozi wa mkoa wa Morogoro na wafanyabiashara wa mkoni humo kuangalia namna ambavyo wanaweza kuwasaidia wahanaga hao.
Aliwaomba wananchi kwa ujumla nchini, kuona maafa hayo si ya wilaya ya Kilombero,na mkoa wa Morogoro pekee na kwamba, yanamgusa kila mwananchi bila kujali ni mkazi wa eneo gani.
Akisoma mahitaji muhimu kutokana na mafuriko hayo kwa wafanyabiashara hao kaimu katibu Tawala wa mkoa wa Morogoro, Stephen Bushir aliyataja kuwa ni tani za mahindi 239.14, maharage tani 59.7, mafuta ya kula lita 38,861, chumvi kilo 1438, na sukari kilo 23,000 na kwamba mahitaji hayo ni kwa siku 90.
Alisema mahitaji mengine ni mbegu za mazao yanayokomaa kwa muda mfupi na kutaja kuwa ni mahindi ya muda mfupi tani 6 pamoja na vipando vya mbegu ya muhogo mizigo 14,950.
Kaimu huyo alisema kuwa mafuriko hayo yameathiri miundo mbinu ya barabara yakiwemo madaraja 6, na kwamba kila daraja moja linahitaji kiasi cha shilingi milioni 35, ili liweza kukamilika wakati yote yanahitaji kiasi cha shilingi milioni 210 ili yakamilike.
Alisema kwa upande wa barabara shilingi milioni 340 zinahitajika kwa ajili ya ukarabati wa barabara zenye urefu wa kilomota 34, wakati fedha ya matengezo ya barabara ya Ifakara Taweta ambayo haipitiki kwa sasa kutokana na kuharibiwa vibaya na mafuriko hayo inahitaji kiasi cha shilingi milioni 949.4.
Jumla ya kata nne za Mofu, Mbingu, Mngeta na Ideta wilayani Kilombero zimehabiwa vibaya na mvua zilizonyesha kuanzia Aprili 20 mwaka huu na kusababisha watu 6,643 kukosa makazi.
Katika mafuriko hayo nyumba 673 zilibomoka na 777 kuzingirwa na maji na hekta 596 zikiwa zimeathiriwa na mafuriko pamoja na upotevu wa mali na vyakula vya wakazi wa kata hizo.

No comments:

Post a Comment