Friday, 29 April 2011

HABARI YATINGA FAINALI IKIIZIMA ZECO.

Habari yatinga fainali ikiizima ZECO

Na Mwajuma Juma
TIMU ya soka ya Wizara ya Habari, imefanikiwa kuingia fainali ya mashindano ya 'May Day', baada ya kuilaza Shirika la Umeme (ZECO) mabao 5-2 katika mchezo wa nusu fainali ya kwanza uliochezwa juzi kwenye uwanja wa Amaan nje.
Katika mchezo huo uliochezwa juzi, wakata umeme walionekana kuzidiwa mno na kushindwa kutumia koleo na pakari zao kuwakatia umeme vijana hao wa Habari Sports ambao hivi juzi tu wametoka katika mashindano ya NSSF walikoishia robo fainali.
Vijana wa Habari ambao walionesha mchezo mzuri na soka la kufundishwa, walifungiwa magoi yao na Amour Nassor (mawili)i, Ramadhan Khamis, Abdulghani Mussa na Yussuf Saleh.
Magoli yote ya ZECO katika patashika hiyo, yalipachikwa kimiani na mchezaji Mussa Hassan.
Hata hivyo, hatima ya Habari Sports kama itacheza fainali au la, itajulikana baada ya kusikilizwa rufaa iliyokatwa na wapinzani wao waliodai kuwa timu hiyo ilichezesha majeshi ya kukodi (mamluki).
Michuano hiyo inayoshirikisha timu za mashirika na wizara za serikali, imeandaliwa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC), ikiwa sehemu ya maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani 'May Day', ambapo fainali yake itachezwa keshokutwa siku ya kilele cha sherehe hizo.

No comments:

Post a Comment