Polisi Bridge yatoswa bandarini
Na Mwajuma Juma
MAAFANDE wa timu ya Polisi Bridge, juzi walikiona cha moto baada ya kuzamishwa na Bandari kwa kichapo cha mabao 3-2 katika mchezo wa ligi daraja la kwanza kanda ya Unguja uliochezwa Mao Tsetung.
Magoli ya Bandari yalipachikwa kimiani na wachezaji wake Haitham Khamis aliyefunga kwa penalti mnamo dakika ya 64 pamoja na Mgaza Muhaya (dk 72), na lile la tatu likitiwa kimiani na Fauzi Ali katika dakika ya 77.
Kwa upande wake, Bridge ilifungiwa mabao yake na Khamis Ali (dk 69) na Ali Othman kwa njia ya penalti kufuatia nahodha wa timu ya Bandari Haitham Khamis kumchezea rafu Ali Haji.
Hata hivyo, Bandari ilipata pigo baada ya mchezaji wake Hussein Suleiman kutolewa nje kwa kadi nyekundu kufuatia kumtolea lugha chafu muamuzi Mgaza Kinduli.
Na katika mchezo mwengine, maafande wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania timu ya Kipanga, iliichezesha kwata timu ya Mlandege kwa kuifunga magoli 3-1.
Walioifungia Kipanga katika mtanange huo, ni Ali Abdallah ( dk 7 na 64), huku Abuu Hemed akipachiia la tatu katika dakika ya 78, ambapo Mlandege ilijifariji kwa goli la Mohammed Abdallah Golo alilolifunga mnamo dakika ya 71.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena leo kwa mchezo kati ya Mtende Rangers na Sharp Boys.
Friday, 8 April 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment