Tuesday, 26 April 2011

MBUNGE AJITOLEA KUWALIPA FAINI WAFUNGWA MAHABUSU

Mbunge ajitolea kuwalipia faini wafungwa, mahabusu

Na Nalengo, Morogoro
MSICHANA aliyefungwa kwa kushindwa kulipa faini kwenye gereza kuu la Morogoro mjini, Nasra Ramadhani anayekadiriwa kuwa na umri kati ya (13-15) mkazi wa Chamwino Manispaa ya Morogoro amemtia Simanzi Mbunge wa jimbo la Morogoro mjini Abdulaazizi Abood, na kulazimika kutoa shilingi milioni 7 kuwalipia faini aliyoshindwa kulipa.
Mbunge huyo alisema atatoa kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kuwalipia faini wafungwa 50 waliofungwa, baada ya kushindwa kulipa faini, ili kupunguza msongamano wa wafungwa kwenye gereza hilo.
Wafungwa watakaolipiwa ni wale waliotakiwa kulipa faini na kushindwa, kuanzia kiasi cha shilingi 10,000 hadi 120,000, na kwamba msamaha huo ni pamoja na msichana huyo.
Kauli hiyo aliitoa mjini hapa wakati alipofanya ziara ya kutembelea gereza hilo kwa ajili ya kusikiliza kero za wafungwa na mahabusu, soko kuu pamoja na kuongea na askari polisi, ambapo alibaini kuwepo kwa idadi kubwa ya wafungwa na mahabusu kwenye gereza hilo na kusababisha kuwa na msongamano.
“Baadhi ya wafungwa wamefungwa kwa kushindwa kulipa faini ya shilingi 10,000, 70,000, na wameniahidi kuwa hawatarudia tena kufanya makosa, wanasema wamejifunza, nimeona ni bora niwalipie faini ili watoke wapunguze msongamano”, alisema Mbunge huyo.
Abood alisema gereza hilo ambalo linauwezo wa kuwa na idadi ya mahabusu 144 kwa sasa lina mahabusu 565, kiwango ambacho ni kikubwa na kuweza kuhatarisha wa afya zao.
Aidha Mbunge huyo alisema kuwa mahabusu hao wamekuwa wakilalamikia ucheleweshwaji wa kesi zao na kwamba zinakaa sana mahakamani, ambapo baadhi yao wamemwambia kuwa kesi zao zina miaka sita hazijasikilizwa.
Alisema baadhi ya mahabusu hao wamelalamikia kukosa dhamana kutokana na kukosa wadhamini ambao ni watumishi serikalini, na hivyo kuomba kesi ambazo ni nyepesi wapewe dhamana ili kupunguza msongamano wa mahabusu kwenye gereza hilo.
Kwa upande wake mkuu wa Gereza hilo, Mwaluka Dugange alimwambia Mbunge huyo kuwa gereza hilo linakabiliwa na changamoto mbalimbali na kuzitaja baadhi kuwa ni ukosefu wa vifaa vya kupikia na kwamba masufuria yaliyopo yamepasuka.
Alisema kutokana na msongamano uliopo masufuria hayo yanashindwa kuhimili kupika chakula cha watu 565, pamoja na uhaba wa maji na kwamba hayatoshelezi kutokana na msongamano huo.

No comments:

Post a Comment