Thursday, 14 April 2011

KUNGURU 400,000 WATEKETEZWA ZANZIBAR.

Kunguru 400,000 wateketezwa

Na Mwantanga Ame

ZOEZI la uuaji kunguru linaloendeshwa na wizara ya Kilimo na Maliasili, limefanikiwa kuwaua ndege hao 400,000 tangu kuanza kwake.
Zoezi hilo linaloendeshwa katika maeneo yote ya Unguja na Pemba, ikiwa ni hatua ya kupambana na ndege hao baada ya kuonekana kuongezeka kwa idadi kubwa na kusababisha kutokea kwa uharibifu katika maeneo mbali mbali ya Mjini na Vijijini.
Baadhi ya Maofisa wa wizara hiyo walilieleza Zanzibar Leo kuwa ndege hao wamekuwa wakisababisha uharibifu mkubwa katika vyombo vya mawasiliano hasa kwenye minara ya simu.
Maofisa wanaohusika na zoezi hilo walieleza kuwa ndege hao tayari wameshaitia hasara kampuni ya simu ya ZANTEL ya shilingi milioni 30 kwa nusu saa ya kukosekana mawasiliano baada ya kuchomoa moja ya kifaa muhimu katika minara hiyo.
Aidha, maatatizo mengine yanayotokana na ndege hao walieleza ni pamoja na uharibifu wa mazao na kuiba vitu majumbani huku wakichafua mazingira kutokana na kuiba mabendeji yanayotupwa katika taka taka za mahospitali binafsi na kusambaza mitaani.
Aidha ndege hao wamekuwa wakiwasumbua wanyama hasa ng’ombe kwa kutafuna pale wanapowagundua kuwa na vidonda.
Akizungumza na waandishi wa Habari, Naibu Katibu Mkuu wa Maliasili Dk. Bakari Asseid, alisema tangu wameanza zoezi hilo tayari kunguru 400,000 wameshauliwa.
Alisema mradi huo ambao unatekelezwa chini ya mfuko wa MACEMP lengo lake ni kuuwa kunguru milioni 1/= kwa Unguja na 900,000 kwa Pemba lakini madhumuni ni kuuwa kunguru wote.
“Lengo ni kuuwa kunguru wote waliopo Unguja na Pemba kama atabakia mmoja basi huyo tunaweza tukamfanyia sherehe ya kuwa kunguru wa mwisho kuuawa”, alisema Dk. Aseeid.
Alisema katika kuteketeza kunguru hao kitengo husika kimekuwa kikitumia nyama ambayo huwekewa sumu ambayo haina madhara kwa binadamu na kuwekwa katika mapaa na baadae huondolewa.
Hapo awali Zanzibar Leo ilipozungumza na msimamizi wa mradi huu katika kituo cha Mazao ya biashara na Misitu Maruhubi Zanzibar, Yussuf Kombo, alisema jumla ya fedha zinazotarajiwa kutumiwa kwa kazi hii ni shilingi milioni 163 na hadi mienzi miwili iliyopita walikuwa tayari wameshatumia shilingi milioni 12.

No comments:

Post a Comment